ILIANZA kama tetesi vile, lakini taarifa zikufikie kwa sasa kwamba Mnyama amemalizana na kiungo mkabaji, Augustine Okejepha aliyekuwa akikiichezea Rivers United ya Nigeria.
Mwanaspoti liliripoti hivi karibuni juu ya dili hili la Simba na Mnigeria huyo anayetajwa kuja kuchukua nafasi ya Babacar Sarr anayetarajiwa kupewa ‘thank you’ muda wowote kuanzia sasa ili kupisha majembe mengine mapya kuingia Msimbazi.
Tayari Simba imeshatangaza kuchana na wachezaji wanne, akiwamo aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco, Shaaban Idd Chilunda, Saido Ntibazonkiza na Kennedy Juma na imeshamtambulisha beki wa kati, Lameck Lawi kutoka Coastal Union.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti, kuwa mazungumzo kati ya Simba na kiungo huyo yamefikia katika hatua Nzuri na mchezaji yupo tayari kusaini mkataba wakati wowote kuanzia sasa.
“Ni kweli Simba inafanya mazungumzo na kiungo huyo mkabaji na mambo yamekwenda vizuri muda wowote atasaini mkataba kwa kuja kuitumikia msimu ujao,” kilisema na kuongeza;
“Mazungumzo ya pande zote mbili yamekwenda vizuri kilichobaki ni kusainiwa kwa mkataba inaekezwa mchezaji huyo ni mzuri kucheza eneo kiungo mkabaji lakini pia anaweza kucheza beki ya kati.”
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, kiungo huyo atapewa mkataba wa miaka mitatu kutokana na umri alionao, faida ya kucheza zaidi ya nafasi moja uwanjani, kwani mbali na kiungo lakini anamudu pia beki na hilo limewavutia zaidi Simba kwa kuamini ataisaidia timu hiyo endapo nafasi ya beki itakosa mtu.
“Mchezaji huyo ana miaka 20 tu na amekuwa mchezaji mzuri katika kikosi cha Rivers akiwa panga pangua kikosi cha kwanza ubora wake utaongeza chachu kwenye kikosi chetu ambacho tunakisuka sasa.”
Ujio wa kiungo huyo mkabaji ndani ya Simba utamfanya aungane na Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute ambaye inaelezwa kuwa anaweza kaachwa dirisha hili na Mzamiru Yassin wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Pia kuna wazawa wawili wanaotajwa kumwaga wino akiwamo Yusuf Kagoma na Omary Omary walikuwa wakizitumikia Singida FG na Mashujaa mtawalia.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia juu ya dili hilo la Mnigeria alisema huu ni msimu wa usajili kila mchezaji anatajwa kutua Simba, ila hawapo tayari kujibu kila swali kuhusu usajili kwa sasa zaidi wanawaachia viongozi wao wafanye kazi yao muda ukifika zoezi la kutangaza wachezaji walio wasajili likifika watafanya hivyo.
“Hili ni dirisha la usajili mengi yanazungumzwa nikisema nizungumzie kila mchezaji anaetajwa kutua Simba nitachoka. Naomba hili tuliache kwanza muda wa kutambulisha wachezaji tuliowasajili utafika tutafanya hivyo,” alisema Ahmed aliyekaririwa hivi karibuni akisema ‘thank you’ za Simba zinaendelea baada ya kumtambulisha Lawi.