Kila baada ya muda, bao hufungwa kwenye mashindano ya mataifa ya Ulaya huko Ujerumani. Na historia inaandikwa.
Historia ya Lamine Yamal kuifungia Uhispania dhidi ya Ufaransa katika nusu fainali ya Euro 2024, inaweza kuongezwa kwenye orodha ya historia.
Uhispania ikiwa nyuma kwa bao 1-0, Yamal alifunga bao zuri kutoka nje ya eneo la hatari na kumuweka kwenye vitabu vya historia.
Akiwa na umri wa miaka 16 na siku 362, amekuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika historia ya mashindano hayo, na kuwafanya wale waliokuwa wakitazama wabaki na mshangao.
“Mchezaji nyota amezaliwa,” mshambuliaji wa zamani wa Uingereza Gary Lineker alisema kwenye BBC One. “Ni tukio kubwa katika mechi, huenda ni kubwa katika mashindano.”
“Inavutia,” alisema mshambuliaji wa zamani wa Uingereza Alan Shearer. “Tumekuwa tukimzungumzia katika mashindano haya na tukasema ana umri mdogo sana.”
Bao hilo lilishangiliwa na mashabiki ndani ya Allianz Arena na kote duniani, huku likirudiwa kwa mwendo wa taratibu, ni la kuvutia sana kwa sababu ya muda wake.
Iikuwa 1-0, Ufaransa ikiongoza mbele ya Hispania katika nusu fainali ya mashindano makubwa huko Ujerumani.
Yamal alikuwa akitabasamu na kufanya mzaha na wachezaji wenzake uwanjani saa chache kabla ya mchezo kuanza, na akabeba imani hiyo katika uchezaji wake.
“Lilikuwa goli zuri sana,” bosi wa Uhispania Luis de la Fuente alisema kuhusu bao la Yamal.
“Anaonekana ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa kusema ukweli. Ninafuraha kuwa yuko kwenye timu yetu, kwamba yeye ni Mhispania.”
“Tunamtegemea na tunatumai tunaweza kuwa nae kwa miaka ijayo.”
Pia alishaandika historia
Yamal sasa anacheza soka la kimataifa, lakini tayari alikuwa ameandika rekodi katika msimu wake wa mafanikio akiwa Barcelona.
Alikuwa mfungaji mabao mdogo zaidi wa timu ya Uhispania, na pia mfungaji mdogo zaidi kwenye ligi ya La Liga.
Yamal atatimiza umri wa miaka 17 tarehe 13 Julai, siku moja kabla ya fainali ya Euro 2024, ambapo Uhispania itamenyana na England au Uholanzi.
Akieleza kuhusu alitakalo, kijana huyo anasema anachotaka ni kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa “kushinda, kushinda, kushinda na kushinda.”
Yeyote ambaye Uhispania itakabiliana naye kwenye fainali, watapaswa kutompa kijana huyo kiburi kama vile Ufaransa walivyofanya.
Kabla ya mchezo huo, kiungo wa Ufaransa Adrien Rabiot alisema Yamal atahitajika, “kuonyesha zaidi ya alichokionyesha sasa kwenye michuano hiyo.”
Mwishoni mwa mchezo, Yamal alisherehekea kwa kusema mbele ya kamera ya TV: “Zungumza sasa, zungumza sasa.”
Mlinzi wa zamani wa Uingereza Rio Ferdinand alisema: “Ni kama vile Yamal alimuona Rabiot na macho yake yakaangaza na akasema: ‘Nitakuonyesha.’
“Goli zuri kutoka kwa mtoto mdogo sana.”
Yamal alijitokeza katika mkutano wa waandishi wa habari baada ya mechi, wakati vijana wengine wengi wa miaka 16 wakiwa wamelala fofofo, na aliulizwa kuhusu kauli yake inamlenga nani.
“Mtu ninayemzungumzia, atajua mtu huyu ni nani,” alisema.
Akili yake sasa inahamia kwenye fainali ya Jumapili huko Berlin.
“Ni ndoto yangu kufika fainali na timu ya taifa.”
Alipoulizwa ni timu gani angependelea kukuta nayo, alijibu: “Sijali sana. Tutasubiri na kucheza na yeyote yule.”