Sunday, June 21, 2020

Simba yalipa Kisasi kwa Mwadui Taifa na kutandaza soka safi

Tags

Simba yalipa Kisasi kwa Mwadui Taifa na kutandaza soka safi

empty:news-banner-img

Simba yalipa Kisasi kwa Mwadui Taifa na kutandaza soka safi


Mchezo wetu wa ligi kuu dhidi ya Mwadui FC uliopigwa uwanja wa Taifa umemalizika kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku tukionyesha kandanda safi la kuvutia. Mechi hii ilikuwa ni ya kisasi kutokana na mzunguko wa kwanza Mwadui kutufunga kwa bao moja katika uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga hivyo tulipaswa kuhakikisha tunachukua pointi zote tatu. Kiungo mshambuliaji Hassan Dilunga ndiye aliyetufungulia karamu ya mabao kwa kufunga la kwanza dakika ya nane baada ya kazi nzuri iliyofanywa na nahodha John Bocco. Mlinzi Augustino Samson alijifunga na kutupatia bao la pili dakika ya 21 katika jitihada za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe ndani ya kisanduku cha sita. Bocco alitufungia bao la tatu dakika ya 57 kufuatia shuti kali lililopigwa na Luis Miquissone kugonga mwamba wa juu na mpira ukamkuta nahodha ambaye aliumalizia kwa kichwa. Kocha Sven Vandenbroeck aliwatoa Bocco, Dilunga, Miquissone, Kapombe na Gerson Fraga na kuwaingiza Clatous Chama, Medie Kagere, Francis Kahata, Yusuph Mlipili na Mzamiru Yassin ambao nao waliendelea kucheza soka safi lililowavutia mashabiki. Ushindi huu umetufanya kufikisha pointi 75 tukiendelea kuongoza kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 30.