Sunday, June 28, 2020

Simba kuingia na mbinu za Mbeya City kuimaliza Prisons kesho

Tags

empty:news-banner-img

Simba kuingia na mbinu za Mbeya City kuimaliza Prisons keshoKocha Mkuu, Sven Vandenbroeck ameweka hadharani mbinu atakazotumia katika mchezo wa kesho dhidi ya Prisons kuwa ni kama alizotumia katika mchezo dhidi ya Mbeya City Jumatano wiki hii.


Katika mechi hiyo, Sven alitumia mipira ya juu kutokana na Uwanja wa Sokoine kutoruhusu soka la pasi fupi ambalo tumelizoea kutokana na eneo lake la kuchezea (pitch) kutokuwa zuri. "Tutatumia mipira mirefu kama tulivyofanya katika mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, hatutacheza soka la pasi za chini kama kawaida yetu kwa kuwa hali ya uwanja haituruhusu kufanya hivyo," amesema Kocha Sven. Simba imekuwa ikisifika kwa soka safi la pasi za haraka za chini lakini Kocha Sven ameamua kubadili mfumo huo ili kuendana na hali ya Uwanja. Licha ya kuweka wazi kuwa atatumia mfumo wa mipira mirefu kocha Sven ameahidi kucheza soka safi la kuvutia kama ilivyo kawaida ya timu yetu. Kuhusu hali ya kikosi kocha Sven amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na wapo tayari kwa mchezo isipokuwa kiungo Jonas Mkude ambaye anamalizia adhabu yake ya kufungiwa mechi mbili. "Wachezaji wote wako vizuri wana ari tayari kwa mchezo wa kesho, isipokuwa tutaendelea kumkosa Mkude ambaye anamalizia adhabu yake ya kukosa mechi mbili," amesema kocha Sven