Wednesday, June 24, 2020

Simba Kamili kuivaa Mbeya City Leo Sokoine

Tags

empty:news-banner-img

Simba Kamili kuivaa Mbeya City Leo Sokoine


Kikosi chetu leo kitashuka katika uwanja wa Sokoine jijini hapa kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City kikiwa kamili tayari kwa kuzisaka pointi tatu. Tunaingia kwenye mtanange huu tukiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 4-0 tuliopata kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza. Mchezo huo ambao ulipigwa Novemba 3 mwaka jana katika uwanja wa Uhuru mabao yetu yalifungwa na Medie Kagere kwa mkwaju wa penati, Clatous Chama, Sharaf Eldin Shiboub na Deo Kanda. KAULI YA KOCHA SVEN Kuelekea mchezo wa leo kocha, Sven Vandenbroeck amesema wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri na kila mmoja yupo tayari ingawa amekiri mechi itakuwa ngumu. "Wachezaji wote wapo vizuri kimwili na kiakili, tunategemea kupata ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani ukizingatia watakuwa nyumbani lakini lengo letu ni lile lile pointi tatu," amesema kocha Sven. NAHODHA NAE ATOA NENO Nahodha wa timu John Bocco 'Adebayor' amesema wanafahamu mchezo utakuwa mgumu lakini lengo la kwanza itakuwa kuhakikisha tunapata pointi zote tatu. "Tunafahamu mechi itakuwa ngumu kwakua kila timu inahitaji pointi tatu katika kipindi hiki ligi ikielekea ukingoni lakini sisi tumejipanga kukabiliana chochote kitachotokea ili kupata pointi tatu," amesema Bocco. Matokeo ya mechi saba zilizopita kati yetu na City Simba 4-0 Mbeya City Mbeya City 1-2 Simba Simba 2-0 Mbeya City Simba 2-2 Mbeya City Mbeya City 0-2 Simba Simba 2-0 Mbeya City Mbeya City 0-1 Simba