Yanga: Waleteni hao Township Rollers tumeiva

Yanga: Waleteni hao Township Rollers tumeiva

YANGA imekamilisha programu yake ya mazoezi visiwani Zanzibar kuelekea mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana itakayopigwa Uwanja wa Taifa kesho na kueleza sasa mambo ni moto na ipo tayari kwa mechi hiyo ya kimataifa.
Baada ya kuhitimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi Jumapili kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kariobangi Sharks ya Kenya katika Uwanja wa Taifa, Yanga ilielekea Zanzibar kuweka kambi ya muda mfupi na kucheza mechi mbili za kirafiki ikianza na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mlandege juzi kabla ya jana usiku kuhitimisha kwa kuvaana na Malindi FC kwenye dimba la Amaan.

Kwa mazoezi waliyoyapata, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, alinukuliwa akieleza kuwa hana wasiwasi na kikosi chake kwa sasa na anaamini kitampa matokeo chanya kimataifa.

 Zahera alisema anaona namna kikosi chake kilivyozidi kuimarika baada ya mechi yake dhidi ya Kariobangi Sharks na ile ya Mlandege, hivyo ana anaimani kitapata matokeo chanya kwenye michezo ya kimataifa.

"Kwa tulipofikia si sehemu mbaya, kila mmoja ana morali ya kufanya kazi na kutimiza majukumu yake uwanjani.

"Tunatambua kwamba ipo kazi ya kucheza kimataifa, hilo halitupi taabu tumejiandaa na mashabiki watupe sapoti ili tufanye vizuri," alisema.

Akizungumzia mechi dhidi ya Mlandege, ambayo walishinda mabao 4-1 juzi, Zahera licha ya kuvutiwa na namna wapinzani wao walivyocheza kwa kasi licha ya kupoteza, alisema walipata mazoezi mazuri kutokana na kasi ya wapinzani hao.

Alisema kasi waliyonayo Mlandege imewapa mazoezi na maandalizi mazuri kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers.

Katika mechi hiyo, Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa nyota wa kigeni, Mnyarwanda Patrick Sibomana dakika ya 26, hilo likiwa ni bao lake la pili tangu ajiunge na Yanga, la kwanza likiwa ni dhidi ya Kariobangi Sharks alilofunga kwa mkwaju wa penalti.

Mabao mengine yalifungwa na Mganda Juma Balinya dakika ya 36, Mnamibia Sadney Urikhob dakika ya 42 na mzawa Mrisho Ngassa dakika ya 65, huku bao pekee na la kufutia machozi la Mlandege likifungwa na Hassan Bamzu dakika ya 88.

Katika hatua nyingine, wakati Yanga ikitarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo ikitokea Zanzibar, wapinzani wao kimataifa, Township Rollers walitarajiwa kutua nchini jana tayari kwa mechi hiyo ya Jumamosi.

Yanga ikipata matokeo ya jumla katika mechi hiyo na ile ya marudiano itakayopigwa nchini Botswana kati ya Agosti 23-25, mwaka huu, itakutana na mshindi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia Nipashe jana, Yanga imefanikiwa kuingiza Sh. milioni 283 na ushee katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, fedha hizo zikitokana na kiingilio cha idadi ya mashabiki 48,630 walioingia uwanjani siku hiyo.

Wakati Simba yenyewe ikivuna Sh. milioni 376 na ushee kutokana na mashabiki 58,001 walioingia Uwanja wa Taifa kilele cha Simba Day juzi Jumanne.