Yanga, Township patachimbika Taifa

Yanga, Township patachimbika Taifa
KAMA Township Rollers ya Botswana wanatarajia mteremko kwa Yanga kesho kwenye mechi yao ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika , basi pole yao kwani wenyeji wao wamepania kulipa kisasi cha mwaka jana watakapokabiliana Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Kocha msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila alisema mchezo huo una umuhimu mkubwa kwao kutokana na kuanzia nyumbani.
"Mchezo huu ni mkubwa kwetu na hatuna cha kupoteza zaidi ya kuhitaji kupata matokeo mazuri, tupo nyumbani na tuna kila sababu ya kushinda," alisema.
Alisema anafahamu ugumu wa mchezo huo lakini anawaamini wachezaji wake watafanya kitu cha tofauti kupitia maandalizi waliyofanya.
"Tumekuwa na wiki takribani nne za kujiandaa na mchezo huu, kwahiyo kuna wachezaji wapya ambao wameingia na wameshakopi na wenzao naamini tutafanya kitu tukiwa nyumbani," alisema.
Akizungumzia upande wa wapinzani wao ambao walikutana nao mara ya mwisho na kuchezea kichapo, alisema timu hiyo imebadilika wachezaji na sio walewale waliokuwepo.
"Timu zote zimebadilika wachezaji, waliokuwa Yanga na waliokuwa Township sio wale wale kwahiyo kila timu ina wachezaji wapya muda huu," alisema.
NayeKocha wa Township Rollers, Thomas Trucha alisema anatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na kuwa ugenini bila kuwa na mashabiki wao.
"Tupo ugenini tunacheza mechi ngumu, sina uhakika kama tutakuwa na mashabiki lakini tutapambana tukiwa hapa," alisema.
Akizungumzia upande wa mchezo husika na wapinzani wake, alisema amekuwa akiwafatilia hivyo ni timu anayoifahamu.
"Nimeifuatilia Yanga katika baadhi ya michezo waliyocheza, nimejua namna ambavyo wanacheza lakini vilevile haa vipande vya michezo yao nimevifatilia, kikubwa tukutane uwanjani," alisema Kocha Trucha.
Mwaka jana kwenye mechi ya michuano hiyo raundi ya kwanza, Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 toka lwa Township kabla ya kwenda kulazimishwa suluhu ugenini na kung'olewa ikiangukia playoff ya Kombe la Shirikisho na kutinga makundi kwa kuitupa nje Welaita Dicha ya Ethiopia.