Sunday, August 11, 2019

Waje Kwa Mkapa ndiyo watatutambua- SIMBA

Tags


Waje Kwa Mkapa ndiyo watatutambua- SIMBASimba ikiwaanzisha nyota wanne wapya iliyowasajili hivi karibuni, Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Shiboub Sharaf Eldin na Francis Kahata iliwabana wapinzani wao kwa muda wa dakika 90 na suluhu hiyo imekuwa na faida kwao.


Mbali na kuwapa nafasi ya kutafuta ushindi kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo, lakini suluhu hiyo imeifanya Simba kuandika rekodi ya kutoruhusu wavu wake kuguswa kwa mara ya kwanza katika mechi saba ya michuano hiyo.


Katika mechi sita za msimu uliopita, Simba iliruhusu mechi zote wavu wake kuguswa, ikishinda 4-1 dhidi ya Mbabane Swallows, ikalala 2-1 dhidi ya Nkana Red Devils, ikachakazwa mabao 5-0 katika mechi mbili mfululizo dhidi ya AS Vita na Al Ahly kisha kupigwa 2-0 na JS Souara na kukandikwa mabao 4-1 dhidi ya TP Mazembe.


Simba chini ya Kocha Patrick Aussems ilianza pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa HCB mjini Beira kwa kasi, lakini wenyeji wao waliwabadilikia kwa kufanya mashambulizi makali langoni mwa vijana wa Msimbazi na kuwapa kazi mabeki Erasto Nyoni na Pascal Wawa kufanya kazi ya ziada.


Kipa Kakolanya, aliyekuwa akiichezea Simba kwa mara ya kwanza katika mechi za mashindano akitokea Yanga, alifanya kazi nzuri kuokoa michomo kadhaa ya washambuliaji wa Msumbiji, huku Shiboub, Meddie Kagere na Kahata wakitengeneza nafasi.


Katika kipindi cha kwanza Simba walikuwa wanacheza kwa kupoteana eneo la katikati lililokuwa na Francis Kahata, Sharaf Shiboub na Jonas Mkude wakikosa uelewano ndani ya dakika 12 za mchezo huo.


Simba walikuwa wakicheza kwa kujihami hali ambayo walijikuta wakiwa nyuma bila kufanya mashambulizi, lakini pia hali hiyo iliwasaidia kwasababu washambuliaji wa UD Songo walikuwa wanashindwa kupenya ngome ya Simba na kuanza kupiga mashuti ya mbali.


Simba walianza kushambulia dakika 28, lakini kila walipokuwa wanajaribu kuingia na kushambulia walikuwa wanakutana na vizingiti kutoka katika safu ya ulinzi ya UD Songo.


Kipindi cha pili Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa Chama na nafasi yake ilichukuliwa na Mzamiru Yassin, wakati huo huo dakika 71 alitolewa Kahata na kuingia Deo Kanda.


Mabadiliko hayo yalifanyika kwa lengo la kuongeza nguvu katika eneo la kiungo ambalo lilionekana wenyeji wakitawala wakitumia nguvu nyingi na akili.


Dakika 77 Simba walikaribia kufunga bao baada ya Kagere kupiga krosi fupi ambayo kiungo Shiboub aliiunganisha kwa kichwa na kipa wa Ud Songo aliucheza mpira huo kiushujaa na kuwa kona isiyokuwa na faida.


Simba walifanya mabadiliko mengine katika eneo la kiungo dakika 80 kwa kumtoa Jonas Mkude na kumuingiza Hassan Dilunga, mabadiliko hayo yalionyesha kuweka tija.


Simba imerejea usiku wa kuamkia leo tayari kwa mchezo wa marudiano huku wakijivunia rekodi ya kupata matokeo mazuri nyumbani kwenye michuano hiyo, kwani katika mechi sita ilishinda tano na kutoka sare moja na kutinga robo fainali.


Simba ilizifunga Mbabane Swallows kwa mabao 4-0, ikaichapa Nkana 3-1, ikainyuka JS Saoura kwa mabao 3-0, kisha ikailaza Al Ahly 1-0 na kuichaza AS Vita mabao 2-0 kabla ya kulazimishwa suluhu na TP Mazembe.