Saturday, August 17, 2019

Toto Akubali Yaishe Yanga

Tags

Toto Akubali Yaishe Yanga

KIUNGO wa Yanga, Feisal Salum Toto amefunguka kuwa kuongezeka kwa wachezaji katika idara ya kiungo kutamfanya azidishe juhudi ili kuilinda nafasi yake ndani ya klabu hiyo.

Feisal alikuwa katika sehemu ya kikosi cha kwanza cha Kocha Mwinyi Zahera lakini kwa sasa kocha huyo ameonekana kuwatumia zaidi Papy Tshishimbi, Balama Mapinduzi na Mohamed Banka katika eneo la kiungo.

Feisal alisema Yanga ni timu kubwa na inahitaji kuwa na wachezaji wengi wenye viwango vikubwa, baada ya ongezeko la
wachezaji anatakiwa kuongeza ubora ili pate nafasi.

“Yanga ni timu kubwa sana na inashiriki michuano mingi, lazima iwe na wachezaji wengi wenye uwezo mzuri wa kupambana na ili mimi nilinde nafasi yangu kwenye kikosi cha kwanza inabidi niongeze uwezo ndani ya Yanga,” alisema kiungo huyo.

Baadhi ya wachezaji walioongezeka katika eneo la viungo ni pamoja na Mapinduzi, Issa Bigirimana na Abdulaziz Makame ambao walisajiliwa kuongeza nguvu katika eneo la kiungo cha Yanga.

Yanga kwa sasa ipo Kilimanjaro ikijiweka sawa kwa ajili ya mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers, utakaofanyika wikiendi ya wiki ijayo Gaborone nchini Botswana.