Friday, August 9, 2019

Simba ifuata UD Songo bila Manula, Ajibu

Tags

Simba bila Manula, Ajibu kwa UD Songo
WAKATI Simba ilitarajiwa kukwea pipa binafsi la kukodi leo asubuhi kuelekea Msumbiji tayari kwa mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo, nyota watatu wa kikosi hicho imeelezwa hawatakuwapo katika msafara huo kutokana kuwa majeruhi.
Wachezaji ambao walielezwa katika taarifa ya Simba jana kuwa hawatasafiri na timu ni kipa Aishi Manula, kiungo Ibrahim Ajibu na mshambuliaji Mbrazil Wilker Henrique da Silva.

Hata hivyo, nahodha wa Simba, John Bocco, amesema hawana wasiwasi kwa kuwa wanatambua kazi kubwa iliyopo mbele yao ni kupambana kupata matokeo kwenye mchezo huo wa kimataifa.

"Kazi kubwa ni kimataifa na kila mchezaji anajua jukumu lake jipya na namna ambavyo anapaswa kufanya, mashabiki wanapenda kuona timu inapata matokeo na sisi tunakwenda kupambana kwa ajili yao na Taifa," alisema.

Naye beki kisiki wa timu hiyo, Shomari Kapombe, alisema kwa sasa yupo fiti na anatumai kufanya vizuri ndani ya Simba kwenye michuano ya kitaifa na kimataifa.

Kapombe ambaye alikuwa anasumbuliwa na majeraha ya mguu kwa muda mrefu, kwa sasa amerejea kwenye ubora wake na alikuwa sehemu ya kikosi kilichocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Power Dynamos ya Zambia wakati Simba ikishinda 3-1 juzi Jumanne.