Sunday, August 11, 2019

Simba, Azam FC zachafua Hali ya Hewa

TagsKLABU za Simba na Azam FC ambazo wikiendi zilikuwa kwenye majukumu ya kimataifa zimeanza kuwachanganya mabosi wa Chama cha Soka Mkoa wa Iringa kwa ajili ya maandalizi ya pambano lao la Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Simba ilikuwa Msumbiji katika mechi yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo wakati Azam leo Jumapili itashuka ugenini kule Ethiopia kupepetana na wenyeji wao, Fesil Kanema katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya mechi hizo timu hizo zitasafiri hadi Iringa kuumana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Uwanja wa Samora na mabosi wa soka wa mkoa huo, wamefunguka namna wanavyokimbizana kwa sasa kuweka mambo sawa kabla ya klabu hizo kuumana.
Mwenyekiti wa chama cha soka Mkoa wa Iringa (IRFA), Cyprian Kuyava alisema mechi hiyo ni fursa ya kipekee kwa mkoa huo kwani ni ugeni mkubwa utakaowapa vijana wao vipato kwa kazi mbalimbali watakazofanya na hivyo wanapambana kuona kila kitu kinaenda poa.
“Ni mara yetu ya kwanza kuandaa mchezo wa Ngao ya Jamii, hivyo tumefanya maandalizi mazuri ya kuhakikisha mabosi wetu wa juu wanafurahishwa, ili tuweze kupata nafasi wakati mwingine,” alisema Kuyava.
Aliongeza fursa walizokuwa wakizipata wajasiliamali wakati wa michezo ya Ligi Kuu, na sasa watanufaika zaidi kutokana na kuzihusisha timu kubwa.