Monday, August 5, 2019

Samatta aanza kutupia KRC Genk

Tags

Samatta aanza kutupia KRC Genk
STRAIKA wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, ameanza kazi yake ya kucheka na nyavu baada ya juzi kutupia bao lake la kwanza la msimu,
lakini bahati mbaya timu yake ya KRC Genk ikajikuta ikichapwa mabao 3-1 na wenyeji, KV Mechelen katika mchezo wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa AFAS- Achter de Kazerne mjini Mechelen, Malines, Samatta alifunga bao hilo dakika ya 45 na akimalizia pasi ya kiungo Mbelgiji Bryan Heynen.

Bao hilo lilikuwa la kusawazisha baada ya KV Mechelen kutangulia kuziona nyavu kupitia kwa Muivory Coast, William Togui dakika ya 18, kabla ya washambuliaji wenzake, Msweden Gustav Engvall kufunga la pili dakika ya 77 na Mbrazil, Igor Alberto de Camargo kutupia la tatu dakika ya 80.

Kwa ushindi huo Mechelen ni kama imelipa kisasi kufuatia kuchapwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa Super Cup Julai 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.

Katika mechi yake ya kufungua msimu, Genk ilianza vema kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kortrijk kwenye Uwanja wa Luminus Arena.

Samatta, 26, kwa bao lake hilo linamfanya sasa kufikisha jumla ya mabao 63 hapo Genk katika mechi 158 za mashindano yote tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).