Mastaa hawa kuzibeba timu michuano ya Caf

MwanzoSoka Mastaa hawa kuzibeba timu michuano ya Caf
KIPUTE cha michuano ya kimataifa kinatarajia kuanza mwishoni mwa wiki hii kwa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwa wawakilishi wetu wanne kuanza kutupa karata zao uwanjani huku Yanga pekee ikianzia nyumbani.

Yanga itaikaribisha Township Rollers katika Uwanja wa Taifa, huku Simba ikikipiga na UD Songo (Ligi ya Mabingwa) wakati KMC itakwaana na AS Kigali ilhali Azam FC ikitifuana na Fasil Kanema (Kombe la Shirikisho).

Hakuna kisichojificha ndani ya timu hizo kwa usajili uliofanywa ni kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao kwa michuano hiyo, na hapa Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa ambao wanatazamwa kama wakombozi kwenye timu hizo.

MEDDIE KAGERE- Simba

Ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita aliyepachika nyavuni mabao 23, na ndiye mchezaji bora wa mwezi wa nane na wa pili. Huyu alikuwa msaada mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita kwa Simba.

Kagere katika orodha ya wafungaji bora alikuwa anashika nafasi ya pili akiwa na mabao sita huku kinara akiwa na mabao saba ambaye ni Moataz Al Mehdi wa Al Nasr ambaye timu yake ilitolewa hatua za awali kabisa kwenye michuano hiyo.

Pia Soma
 Maguire apewa jezi namba tano Manchester United
Maguire apewa jezi namba tano Manchester United
 Mshambuliaji mkongwe Diego Forlan astaafu soka
Mshambuliaji mkongwe Diego Forlan astaafu soka
 Lowry atoboa siri ya Leonard kuondoka Toronto
Lowry atoboa siri ya Leonard kuondoka Toronto
 Familia yamrudisha Rooney England
Familia yamrudisha Rooney England
FRANCIS KAHATA - Simba

Alikuwa kwenye kikosi cha timu ya Kenya kilichoichapa Taifa Stars 3-2 kwenye michuano ya Afcon mwaka huu kule Misri. Huyu ni kiungo tegemeo kwenye klabu yake ya Gor Mahia kama ilivyo kwa Kagere msimu uliopita.

Kahata alitupia bao muhimu kwenye mchezo dhidi ya Super Sports United na kuiwezesha timu hiyo kuvuka hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.

JOHN BOCCO -Simba

Msimu uliopita alifunga mabao 16 kwenye Ligi Kuu, huku safu ya Simba ndio ilikuwa ikiongoza kwa kufumania nyavu kwenye ligi. Amekuwa mchezaji tegemeo wa Simba na mwaka jana kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Mwadui alitupia mawili na kufikisha jumla ya mabao 100.

Kuondoka kwa Emmanuel Okwi kwenye kikosi hicho kunampa nafasi nyingine nahodha huyo wa Msimbazi kufanya yake msimu huu na kuzidi kuwaaminisha mashabiki wao kuwa bado ni tegemeo lao.

MAPINDUZI BALAMA - Yanga

Moja ya usajili ulioonekana kuzungumzwa sana na mashabiki jukwaani katika mchezo wa kirafiki kati ya Yanga na Kariobangi Sharks ni pamoja na Mapinduzi Balama, dogo aliyetua kutoka Alliance FC baada ya kuupigwa mpira mwingi na Kocha Mwinyi Zahera kummwagia sifa nyingi.

Balama alitua Alliance mwaka 2015 akitokea Mtwivila FC ya Iringa wakati timu hiyo ikishiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) na kuisaidia hadi kupanda Ligi Kuu na kufanya makubwa msimu uliopita kiasi cha kumkuna Zahera aliyemhitaji.

FAROUK SHIKALO - Yanga

Kipa huyu amesajiliwa kutoka timu ya Bandari ya Kenya inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo (KPL). Kuondoka kwa Benno Kakolanya ndani ya Yanga kuliwapa nafasi ya kusaka mwingine kwa ajili ya michuano ya Ligi Kuu na ile ya kimataifa.

Shikalo anao uzoefu mkubwa kwenye soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kwani amewahi kuzitumikia timu za Posta Rangers FC, Muhoroni FC, Posta Rangers FC na Tusker FC zote za Kenya.

PATRICK SIBOMANA - Yanga

Yupo kwenye kikosi cha Taifa la Rwanda tangu mwaka 2015, na msimu huu ametua Yanga akitokea Mukura Victory. Katika michezo ya kujiandaa na mwanzo wa msimu alikuwa na mabao manne akifuatwa na Juma Balinya ‘JB’ (3) sawa na Mrisho Ngassa.

Mnyarwanda huyo (22) anayecheza nafasi ya kiungo na Mrundi Issa Birigimana ambaye ni mshambuliaji walikamilimilisha usajili wao kwa kusaini miaka miwili kuitumikia Yanga SC.Sibomana alikuwa mchezaji wa tatu kumwaga wino Yanga baada ya Papy Tshishimbi na Issa Bigrimana kumalizana na timu hiyo.

IDDY SELEMAN ‘NADO’- Azam FC

Azam FC ilikamilisha usajili wa winga huyo kutoka Mbeya City baada ya kocha wa mpya wa kikosi hicho, Etienne Ndayiragije kupendekeza jina la winga huyo kutokana na kufanya vizuri msimu uliopita aliofunga mabao 10.

Nado alikuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa msimu huu kwa kuanguka wino wa miaka miwili kuitumika Azam FC.

SELEMAN NDIKUMANA - Azam FC

Kwa mara ya kwanza kutua katika ardhi ya Tanzania ilikuwa mwaka 2006 alipokuwa akiichezea Simba, hivyo ukongwe na uzoefu wake ni faida kubwa kwa Azam ambayo wiki hii itakuwa ugenini kucheza na Fasil Kanema kwenye Kombe la Shirikisho.

Azam imemnasa kwa kandarasi ya mwaka mmoja kutoka Al Adalah ya Saudi Arabia. Mrundi huyo pia amekipiga kwenye vikosi vya Molde (Norway) na FK Tirana (Albania).

RICHARD DJODI - Azam FC

Msimu uliopita alikuwa kwenye kikosi cha Klabu ya Ashanti Gold na Azam FC imemsajili kiungo huyo wa Ivory Coast kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Djodi anayemudu kucheza nafasi zote za ushambuliaji, alifanikiwa kufunga jumla ya mabao 17 na pasi 13 za mwisho katika mechi 35 alizoichezea Ashanti Gold huku katika mechi 12 za mwisho akipiga manne.

SALIM AIYEE - KMC FC

Kwa sasa yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa na alikuwa tishio kwa Meddie Kagere kwenye mbio za kufukuzia ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita baada ya kumaliza ligi akiwa na mabao 18 huku Kagere akimaliza kinara na mabao 23.

Aiyee alikuwa mfungaji tegemeo kwenye kikosi cha Mwadui kilichomaliza nafasi ya 17 kikiwa na pointi 44 na kikifunga mabao 47.

JUMA KASEJA - KMC FC

Huyu mkongwe ambaye ameitwa kwa mara nyingine kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania na mwishoni mwa wiki aliweza kuokoa michomo miwili ya penati kwenye mchezo dhidi ya Kenya kusaka nafasi ya Chan mwakani.

Mlinda mlango huyo ana uzoefu wa kucheza michezo mingi ya kimataifa kuanzia kwenye klabu hadi timu ya taifa, na hilo litakuwa fahari kubwa kwa timu hiyo inaposhiriki kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya kimataifa.

BASALA BOKUNGU -KMC FC

Mwaka 2016 alikuwa kwenye kikosi cha Simba na sasa ni mara ya pili kurejea nchini kwa Mkongomani huyo anayecheza nafasi ya beki. Pia amewahi kuichezea TP Mazembe na Esperance huku KMC ikimnasa kutoka Groupe Bazano ya Congo.

Mwaka 2017 wakati Simba ikitinga hatua ya fainali Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2, Bokungu ndiye aliyepiga mkwaju wa mwisho na kuifanya Simba kucheza fainali ambayo iliambulia kichapo.
MaoniMaoni Yako