Mdomo wamponza Messi

Mdomo wamponza Messi
Mdomo wamponza Messi
RIO DE JANEIRO, BRAZIL . MDOMO uliponza kichwa Waswahili walisema na ndicho kilichomtokea Lionel Messi baada ya shirikisho la soka la Amerika Kusini (CONMEBOL) kumfungia miezi mitatu supastaa huyo wa timu ya taifa ya Argentina kufuatia kauli yake ya utata wakati wa fainali za Copa America.
Adhabu hiyo inakwenda pamoja na faini ya Pauni 41,000 aliyotozwa kwa kulibwatukia shirikisho hilo kuwa linanuka rushwa.
Supastaa huyo wa Barcelona alilituhumu shirikisho hilo kwa rushwa kufuatia kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu ambayo Argentina ilishinda 2-1 dhidi ya Chile.
Alisema michuano ya Copa America kwa kuwa mwaka huu imeandaliwa na Brazil, shirikisho hilo lilifanya kila liwezalo kuhakikisha kombe hilo linabaki kwa wenyeji na kwamba anajisikia vibaya yeye, taifa lake na mataifa mengine shiriki kwenda kwenye michuano ambayo ilikuwa ni kuwapotezea muda kwa kuwa bingwa alishapangwa.
Alilalamikia Argentina kunyimwa penalti mbili katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Brazil ambayo wenyeji walishinda 2-0. 

Kutona na adhabu hiyo, Messi atakosa mechi za kirafiki dhidi ya Chile (Septemba 5), Mexico (Septemba 10) na Ujerumani (Oktoba 10) – na mechi moja ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia ambayo inatokana na kadi ya pili ya njano aliyoonyeshwa na kutolewa dhidi ya Chile.
Argentina ilijiliwaza kwa ushindi huo dhidi ya Chile ambayo iliwanyanyasa sana baada ya kuwafunga katika fainali mbili mfululizo zilizopita za Copa America.
Sergio Aguero na Paulo Dybala walifunga lakini Messi alitolewa kwa kadi ya pili ya njano katika dakika 37, baada ya kuonekana akidhamiria kumpiga kichwa Gary Medel wakati wa ugomvi na kiungo huyo wa Chile. Medel alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Messi hajawahi kutolewa kwa kadi nyekundu akiwa na klabu yake ya
Barcelona.
Ila alitolewa alipoichezea kwa mara ya kwanza kabisa Argentina wakati akiwa na umri wa miaka 18 alipoingia kutokea benchini dhidi ya Hungary na kuonyeshwa kadi nyekundi sekunde 90 tu tangu aingie uwanjani kwa kumchezea faulo beki.
MaoniMaoni Yako