Monday, August 12, 2019

Martial kubeba mikoba ya Lukaku Man United

Tags

KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema Anthony Martial atakuwa mshambuliaji wake kiongozi msimu huu baada ya kumkabidhi jezi namba 9 baada ya kuuzwa kwa Romelu Lukaku.


Martial kubeba mikoba  ya Lukaku Man United


Kocha huyo amesema kwamba anaamini kwa kiasi kikubwa kwamba Martial atamaliza tatizo la kufunga kwenye kikosi hicho na kuwafanya kutokuwa na ukame wa mabao kama inavyodhaniwa kwa sasa baada ya Lukaku kutimkia Inter Milan.

Kocha huyo anaamini Martial ni mtu sahihi wa kucheza katikati na hapo kwenye fowadi ataunda pacha na Marcus Rashford.

Katika kipindi ambacho Lukaku alikuwa kwenye kikosi hicho, Martial alikuwa akicheza upande wa kushoto.

Mashabiki wa Man United wanafurahia kwa timu hiyo kumpiga chini Lukaku, ambaye katika kipindi cha misimu miwili amefunga mabao 42 akicheza mshambuliaji wa kati.

Ndani ya kipindi hicho, Rashford amefunga mabao 26 na Martial mabao 23, lakini tofauti ni kwamba wawili hao walikuwa wakishambulia kitokea pembeni.

Solskjaer alisema: “Sawa, Rom amekuwa na rekodi nzuri hasa anapocheza mshambuliaji wa kati. Lakini, nina hakika tutafunga mabao ya kutosha tu kutoka kwa Anthony Martial, Marcus Rashford, Dan James na Jesse Lingard."