Saturday, August 17, 2019

Kampuni ya simu, chakula kumwaga fedha Yanga

Tags

Kampuni ya simu, chakula kumwaga fedha Yanga
BAADA ya msoto wa muda mrefu wa kutawaliwa na hali ngumu ya kifedha hasa msimu uliopita, mambo mazuri yanaendelea kutokea ndani ya Klabu ya Yanga, habari ni kuwa idadi ya wadhamini imeendelea kujitokeza kwa ajili ya kufanya kazi na klabu hiyo.

Kwa ufupi ni sawa na kusema neema inaendelea kujitokeza kwa kuwa hivi karibuni klabu hiyo ilichangiwa zaidi ya Sh milioni 900 na wadau mbalimbali katika harambee maalum iliyopewa jina la Kubwa Kuliko.

Kwa sasa klabu hiyo inaendelea na mchakato wa kupata mdhamini mwingine rasmi kuelekea msimu wa 2019/20 unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, na taarifa ni kuwa hadi sasa makampuni mawili yameshatengeneza uhakika wa kuwa sehemu ya wadhamini na kumwaga mamilioni ya fedha.

Baadhi ya makampuni hayo ni GSM na Taifa Gesi ambayo yapo tayari kuwekeza na mazungumzo yanaendelea huku uhakika wa mamilioni ukiwa mkubwa.

Kabla ya udhamini huo, Yanga imekuwa chini ya udhamini rasmi wa Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa ambayo imekuwa msaada mkubwa kwao kwa misimu kadhaa sasa.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, amesema kuwa hadi sasa wamepokea maombi mengi kutoka katika makampuni mbalimbali wakihitaji kuwadhamini ndani ya klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

“Kuna watu ambao tunazungumza nao ili kuidhamini klabu kwa ajili ya msimu ujao, awali brandi ya Yanga ilikuwa chini sana lakini katika siku za hivi karibuni imeonekana kukua, hivyo kuvutia makampuni mengine kwa ajili ya kuwa wadhamini, hiyo imetokana na amani na utulivu uliokuwepo ndani ya klabu yetu kwa sasa.

“Utulivu uliokuwepo umesababisha makampuni kibao kujitokeza yakiwemo ya chakula, mitandao ya simu, teknolojia na wote tumeshazungumza nao na tupo katika hatua za mwisho za kumalizana.

“Hii yote ni kutokana na kutaka kuikwamua Yanga kutoka kwenye utegemezi na kwenda kwenye kujitegemea yenyewe, kama unavyofahamu sekta ya michezo kwa sasa ni biashara ukiachana na kuburudisha, tuna imani ndani ya muda mfupi klabu itakuwa katika hali nzuri,” alisema Mwakalebela.