Friday, August 9, 2019

KAHATA: Kwa Simba hii, mashabiki mtaipenda

Tags

BAADA ya kushuhudia 'nyomi ya kufa mtu' Uwanja wa Taifa wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Power Dynamsos ya Zambia, kiungo mshambuliaji mpya wa Simba, Mkenya Francis Kahata, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuisapoti timu yao ili iendelee kufanya makubwa zaidi.

Mashabiki wa Simba, Jumanne wiki hii walijitokeza kwa wingi na kufanikiwa kuujaza Uwanja wa Taifa huku wengine wakilazimika kuwekewa TV katika Uwanja wa Uhuru ili kushuhudia kilichokuwa kikiendelea siku hiyo ya kilele cha Simba Day, ambayo waliitumia kutangaza nyota wao wa msimu mpya pamoja na kucheza mechi hiyo ya kirafiki.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kahata alisema anaamini kutokana na ubora wa wachezaji wanaounda kikosi hicho, wanaweza kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa na kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara.

"Kinachotakiwa ni kuendelea kushirikiana na kucheza kitimu, pia mashabiki wasichoke kutuunga mkono ili kutupa hamasa ya kufanya vizuri zaidi katika mechi zetu kama walivyofanya leo (Jumanne)," alisema.

Kahata ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Gor Mahia, wakati akiitumikia timu hiyo ya Kenya akiwa na Mnyarwanda Meddie Kagere, walitengeneza ushirikiano mzuri na kuifanya safu yao ya ushambuliaji kuwa tishio na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya.

Na kwa muda mrefu, Kagere alikuwa akitamani nyota huyo kusajiliwa Simba ili waweze kuendeleza ushirikiano wao wa kucheka na nyavu, jambo ambalo mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi hao wanasubiri kuliona likitokea.

Simba ambayo msimu uliopita ilifika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), ilitarajiwa kuondoka leo asubuhi kwa ndege ya kukodi kuelekea Msumbiji tayari kwa kuanza kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi kwa kuivaa UD Songo kwenye mechi ya raundi ya awali.