Kagere aipaisha Simba

Kagere aipaisha Simba
REKODI zinaongea buana! Shughuli ya straika Mnyarwanda Meddie Kagere pale Simba hakuna asiyeifahamu kuanzia bilionea wao, Mohamed Dewji (MO) hadi mashabiki waliofurika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, juzi Jumanne.
Kagere ameanza kusimika ufalme wake kwa wababe hao wa Ligi Kuu Bara, Simba ikiwa ni msimu wa kwanza tu tangu alipotua nchini akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Achana na rekodi za akina Emmanuel Okwi, John Bocco, Amissi Tambwe na wengine pale Simba, Kagere ameandika yake mpya na ambayo inaweza kuchukua miaka mingi sana kuja kuvunjwa.
Juzi Jumanne Kagere alipiga hat trick pale Taifa wakati Simba ikiikandamiza Power Dynamos kutoka Kitwe, Zambia, kwenye ushindi wa mabao 3-1 na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Msimbazi.
Sasa kwa taarifa yako ni kwamba, mabao hayo hayo matatu ya Kagere yamemfanya kufikisha idadi ya mabao 41 katika mashindano yote tangu alipotua Simba kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 120 milioni.
Lakini, mabosi wa Simba wakashtukia jambo na kuamua kumuongezea mkataba mwingine wa miaka miwili kabla ya ule wa awali kumalizika kutokana na kuwasha moto hadi wapinzani wakaisoma namba.

Mabao hayo ambayo Kagere amefunga ni ndani ya msimu mmoja tu, ambapo alipachika mabao 22 kwenye Ligi Kuu Bara na kubeba kiatu cha dhahabu, mabao sita katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Kagame na mechi za kirafiki kila sehemu amefunga matano, Kombe la Mapinduzi (2) huku lingine akitupia kwenye Ngao ya Hisani dhidi ya Mtibwa Sugar.
Hata hivyo, mwenyewe amelieleza Mwanaspoti kuwa kazi ya kufunga ni jukumu lake la kwanza uwanjani ili kusaidia timu yake kupata matokeo mazuri. Alisema dhamira yake uwanjani ni kusaidia timu kutimiza malengo ya kubeba mataji kisha ndio hujiangalia yeye kwa maana ya kusaka tuzo zingine.

"Kiukweli siwezi kuangalia kuwa hii mechi ya kirafiki au mashandano ndio nicheze katika kiwango cha chini hapana, kila mchezo kwangu ni muhimu sana kwa klabu yangu.
"Msimu uliopita nilifunga mabao 41 katika mashindano yote, lakini msimu huu kwa uwezo wa Mungu na timu yetu jinsi ilivyo naona nitafunga zaidi ya mabao 50.
Wakati Kagere akionekana kuwasha moto ndani ya msimu mmoja huku thamani ya mkataba wake ikiwa Sh 120 milioni, huko England wababe wa Old Trafford, Man United wamemuuza Romelu Lukaku kwenda Inter Milan kwa dau la pauni 73 milioni.
Awali, Man United walimnunua Lukaku kwa dau la thamani ya Sh 200 bilioni, lakini mpaka anaondoka jana alikuwa amecheza mechi 66 na kufunga mabao 28 tu.
MaoniMaoni Yako