Saturday, August 3, 2019

Juuko asaini Waydad Casablanca

Tags

Juuko asaini Waydad Casablanca
Juuko asaini Waydad Casablanca
BEKI wa Simba, Juuko Murshid ameripotiwa kutua Wydad Casablanca ya Morocco ambako amedaiwa kusaini  mkataba wa miaka miwili.
Juuko ametua kwenye klabu hiyo ambapo mkataba wake na Simba unamalizika Novemba lakini vigogo hao wamekubali kumwachia baada ya Wydad kununua mkataba huo huku Mkurugenzi Mtendaji wa Simba, Crescetius Magori akikiri kupokea barua ya maombi ya kulipa mkataba wa Juuko uliobaki.
Juuko ambaye ameichezea Simba kwa miaka mitano ameamua kuondoka ndani ya kikosi hicho ambapo uongozi wake umempa baraka zote.
Magori amesema wamekubaliana na uongozi wa Wydad juu ya mkataba uliobaki wa mchezaji huyo ambapo watailipa na kutoa barua ya kumruhusu.
"Ni kweli tumepokea barua rasmi kutoka Wydad ya kumwomba Juuko, tumezungumza nao na wamekubali kulipa muda uliobaki maana Juuko ana mkataba wetu unaomalizika Novemba mwaka huu, lakini hatuna tatizo tumeruhusu watalipa na tutawapa barua rasmi ya kumwachia," amesema Magori.
Tangu kumalizika kwa michuano ya Fainali za Afcon ambapo Juuko alikuwa kwenye kikosi cha timu yake ya Taifa ya Uganda 'The Cranes' hakurudi kujiunga na kambi ya Simba iliyowekwa Afrika Kusini kwa wiki mbili ingawa viongozi wa Simba walimuhitaji kurejea kazini.
Kabla ya kutua Simba, Juuko raia wa Uganda aliwahi kuichezea timu ya Vipers na SC Victoria University za jijini Kampala.
Juuko ni mchezaji wa pili kutoka Uganda kuondoka ndani ya Simba baada ya wiki hii, Emmanuel Okwi kusaini mkataba na timu ya Al-Ittihad Alexandria FC  inayoshiriki Ligi Kuu Misri.