Harmonize Aandika Kujiondoa Rasmi Wasafi

Msanii Rajab Abdul Kahali kwa jina maarufu Harmonize hatimaye ameandika rasmi kwa kundi la Wasafi Classic Baby WCB akitaka kandarasi yake kuvunjwa.

Akizungumza na runinga ya Wasafi, Afisa mkuu Mtendaji wa WCB, Sallam Mendez amefichua kwamba msanii huyo ameandika rasmi kwa kundi hilo akisema anataka kujiondoa.

Sallam amesema kwamba kwa sasa moyo wa msanii huyo haupo tena kwa WCB na ameitisha mkutano na usimamizi wa WCB katika harakati yake ya kukubaliana na hatua hiyo.

"Harmonize kwa sasa moyo wake haupo WCB, kimkataba bado yupo. Kwa nini nasema hivi? Harmonize ameshatuma barua ya maombi ya kuvunja mkataba na yuko tayari kupitia vipengele vyote vya sheria kusitisha mkataba wake na ni kitu ambacho tumependezewa nacho.

Yeye mwenyewe ameridhia na ameomba kikao na uongozi," alisema Sallam.Hata hivyo amesema kwamba mwanamuziki huyo wa wimbo 'My Boo' bado yupo katika mkataba wa WCB na kusisitiza kwamba ingekuwa heri iwapo Harmonise angetoka bila kuzua zahama.

"Sisi kama taasisi ya WCB tuko radhi kwa kile ambacho ataamua, hatuwezi kupinga chochote. Akiamua kufuata maelezo hayo ana baraka asilimia 100 za Wasafi na akitaka kushirikiana na Wasafi wakati wowote tuko wazi. Unajua unapoondoka katika mazingira mazuri inasaidia uhusiano usalie pale pale," alisema kiongozi huyo wa wasafi .
MaoniMaoni Yako