Friday, August 16, 2019

Haji Manara Awaombea Sapoti Yanga

Tags

MSEMAJI wa Klabu ya Simba, Haji Manara amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuungana na wapinzani wao Yanga katika mechi za kimataifa ambapo Yanga watacheza na Township Rollers katika mechi ya marudiano.Manara amefunguka kuwa, mashabiki wa Tanzania wanatakiwa kuwa kitu kimoja katika kuzisapoti Yanga, Simba, Azam FC na KMC ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).Yanga watarudiana na Rollers nchini Botswana, wakati Simba wataivaa UD do Songo, Azam FC watacheza na Fesile Kenema ya Ethiopia na KMC watacheza na AS Kigali.Mechi zote hizo tatu zitachezwa jijini Dar. Manara ameliambia Championi Ijumaa, kuwa viongozi na mashabiki wa soka wanatakiwa kuwa kitu kimoja kwa timu zao kuhakikisha zinafuzu kuingia hatua ya makundi. “Hili ni suala linalohusu taifa hivyo inabidi kuwa kitu kimoja.Nawaomba TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) baada ya mechi ya Ngao ya Jamii (kesho Jumamosi) tuzunguke katika vyombo vyote vya habari kwa ajili ya kuhamasisha hili. “Timu zote zikitinga hatua ya makundi hakika Tanzania itapiga hatua zaidi na tutaendelea kulinda nafasi hii ya timu nne kushiriki michuano hiyo,” alisema Manara.Aidha, Manara ameweka wazi kuwa kuna jezi feki za klabu hiyo ambazo zimeingizwa nchini.“Kuna jezi feki zimeingia hapa nchini zikiwa tofauti na zile zetu, tumeshaandika barua kwa wizara lakini pia tunawataka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) walifanyie kazi sababu tunategemea jezi hizo ili tujiendeshe. Wanaotaka jezi waende wakanunue kwa mawakala wote,” alimaliza Manara.