Gaucho roho kwatu Msimbazi

Gaucho roho kwatu Msimbazi
Gaucho roho kwatu Msimbazi
MSHAMBULIAJI wa Simba Queens, Mwanahamisi Omary 'Gaucho' amesema kitendo cha uongozi wao kuwapeleka kufanya ziara Ujerumani, kimewafungua na kuwapa moyo wa kuona kazi yao inapewa thamani kama ilivyo kwa wanaume.
Mwanahamisi amesema imezoeleka kwenye timu za wanaume kuweka kambi nje ya nchi, huku wao wakipata bahati ya kuvuka mipaka ya Tanzania wakiwa na timu ya taifa 'Twiga Stars', jambo alilodai awamu hii imekuwa tofauti ndani ya Simba Queens.
"Unajua tumechagua soka kuwa maisha yetu, nilianza kucheza nikiwa mdogo na sasa naendelea kukua siku hadi siku, kazi hii ndio natakiwa kujenga maisha yangu, ikikosa kupewa thamani inaumza kupita kiasia," amesema na kuongeza;
"Ukiona mchezaji wa kike amesafiri kwenda Ulaya basi yupo na timu ya taifa ama dada zetu kina Sophia Mwasikili ambao walibahatika kucheza Uturuki, kitendo cha viongozi wa Simba kutupeleka Ujerumani kimebadili mitazamo yetu."
Straika huyo aliwahi kutamba na Mlandizi Queens na kuwapa taji la michuano ya kwanza ya Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2016-17 aliongeza kwa kusema;
"Kila kitu kinahitaji subra kwani hata sisi hatukujua kama tungeenda Ujerumani, hii imetupa mwanga wa namna ambavyo tunahitaji kuiwakilisha rangi nyekundu kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya wanawake Tanzania Bara."