Azam dozi mara mbili Ethiopia

Azam dozi mara mbili Ethiopia
BAADA ya juzi kuwasili salama nchini Ethiopia, wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC wameendelea kujiweka sawa kwa kujifua asubuhi na jioni tayari kwa mechi yao dhidi ya Fasil Ketema (Ethiopia 1) itakayopigwa Jumapili mjini Gondar Kaskazini mwa nchi hiyo.

Azam iliamua kwenda mapema ikiwa ni siku nne kabla ya mchezo wao kwa lengo la kuzoea hali ya hewa ya huko ambayo inaelezwa kwa sasa ni baridi kali.

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya barua pepe kutoka nchini Ethiopia, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jafari Iddi Maganga, alisema, licha ya hali ya baridi, kikosi chao kipo salama na katika mazoezi ya timu hiyo, hakuna mchezaji aliyeonekana kusumbuliwa na hali ya hewa ya Ethiopia.

"Tunashukuru tupo salama leo (jana), tumefanya mazoezi asubuhi na jioni pia tutaendelea kujifua kila siku hadi siku ya mechi kulingana na programu aliyojiwekea kocha wetu Etienne Ndayiragiji," alisema Maganga.

Aidha, alisema kwa mujibu wa kocha huyo mikakati yake ni kuanza kwa ushindi ugenini licha ya kwamba wanatarajia kupata ushindani mkubwa.

"Kocha wetu ameahidi kufanya vizuri kutokana na jinsi alivyokiandaa kikosi chake, kikubwa anaomba dua zenu  huko nyumbani," alisema Maganga.
MaoniMaoni Yako