Simba Yatakiwa Ijisafishe Uchafu Huu Kabla Ya Kuikabili Al Ahly

SIMBA itacheza mchezo wake wa tatu na wa pili ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri ikitoka kupoteza mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo kwa mabao 5-0.
Simba Yatakiwa Ijisafishe Uchafu Huu Kabla Ya Kuikabili  Al Ahly
Mchezo huo dhidi ya Ahly unaweza kuwa muhimu zaidi kwa Simba kutokana na kuhitaji kufuta matokeo mabaya ya mchezo uliopita na kurudisha matumaini katika Kundi D.
Kuelekea mchezo huo utakaopigwa Februari Mosi jijini Cairo, Simba inatakiwa kuanza kujiangalia upya juu ya makosa yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya AS Vita endapo inahitaji matokeo mazuri.
UVIVU WA KUCHEZA KROSI
Safu ya ulinzi ya Simba ilifanya makosa mengi katika mchezo uliopita kipa namba moja, Aishi Manula hakuwa katika ubora wa kucheza mipira ya kona na hata krosi lakini pia hapohapo kuna wakati alilazimishwa kutokuwa na nafasi ya kufanya kazi yake akibanwa na watu wawili waliomkinga.
Endapo Manula ataandaliwa vizuri sambamba na mabeki wa timu hiyo haitashangaza baada ya mchezo huo mchezaji bora wa mechi akatokea eneo hilo, kutokana na Waarabu hao watakavoishambulia sana Simba. Lakini swali litakuja Manula na mabeki wake watakuwa katika ubora wa kuzima mashambulizi hayo?
Alichofanyiwa Manula kilitakiwa kusawazishwa na mabeki kwa kwenda kupambana na watu hao lakini hawakuwa na ubora wa kucheza mipira ya juu makosa hayo yaliifanya Simba kuruhusu mabao mawili ya kona kwa mabeki wa kati wa Vita kufunga kirahisi.
Unapocheza na timu za Kaskazini na ukakosa umakini katika kucheza mipira ya juu utafungwa kirahisi kutokana na kwamba hiyo ndiyo silaha yao kubwa ya kutafutia mabao.
FAULO KARIBU NA BOKSI
Kufanya makosa ya kucheza madhambio karibu na eneo la hatari ni sawa na kusema unahitaji kufungwa, Simba ili waweze kuwabana Waarabu wanatakiwa kumalizana nao mbali na eneo la hatari. Kufanya makosa ya kucheza vibaya karibu na eneo hilo hawatatoka salama Uarabuni kosa kama hili lilifanyika pale Kinshasa lakini mpira wa adhabu wa Jean-Marc Makusu Mundele ukapiga mwamba katika kipindi cha kwanza.
NIDHAMU YA MCHEZO
Waarabu hawataki mpira wa kutumia nguvu, mashambulizi yao yanapita katika njia.
Simba wanatakiwa kuhakikisha akili yao inakuwa sawa kwa kuheshimu nidhamu ya mchezo. Makosa ya faulo za ajabu ajabu kama za Juuko Murushid kadi nyekundu zitahusika na mkishapungua Waarabu ni kama mmewapa njia ya kuwamaliza.
MAFUNDISHO YA AUSSEMS
Wachezaji wa Simba wanatakiwa kuwa na weledi katika mechi hizi kwa kuzingatia ambacho makocha wao hasa Patrick Aussems anawaelekeza. Katika mchezo dhidi ya AS Vita licha ya kuelekezwa juu ya umakini wa kucheza mipira ya juu hususan kona lakini bado wakaruhusu mabao mawili, hili halitakiwi kujirudia katika mchezo ujao.
UVIVU WA KUKIMBIA
Uwanja wa Kimataifa wa Cairo ambao unatumiwa na Al Ahly eneo hilo kuna baridi kali wakati wote wa mchezo. Simba wanatakiwa mapafu yao yawe kamili kwa kuzoea hali ya hewa. Wanachokifanya Al Ahly dakika 20 za kwanza wanakuwa na kasi hilo linatakiwa kuzingatiwa katika maandalizi ya kikosi cha Simba ikitokea kasi hiyo ya Waarabu Simba wakashindwa kuhimili mambo yanaweza kuwa mabaya.
KUTUMIA NAFASI
Simba ilianza vizuri mchezo dhidi ya AS Vita na shambulizi la kwanza hatari katika mchezo huo lilikuwa ni lile la mshambuliaji Meddie Kagere akiwa uso kwa uso na kipa Nelson Lukong lakini kipa akacheza. Nafasi ya namna hiyo ikitokea Simba inatakiwa kutulia na kuitumia vzuri.
NAFASI YA SIMBA KUNDI D
Simba bado ina nafasi kubwa katika kundi lake muhimu ni kutambua katika mechi mbili za ugenini walizobakiza ni vyema kupata pointi sita, tano au hata mbili na sio kupoteza zote.
Ikitokea Simba ikapoteza mechi zote mbili za ugenini itakuwa na presha kubwa kuifunga Al Ahly na AS Vita nyumbani huku ikiomba mechi zao ziishie kwa sare au zifungane,hesabu ambazo ni ngumu.
Simba inayoshika nafasi ya tatu kuvuka katika timu mbili bora katika kundi lake ni kupata pointi zote au hata mbili ugenini lakini hilo lifanyiwe maandalizi makubwa.
Mbali na hilo, Simba inatakiwa kuendeleza makali yake katika mechi zake mbili za nyumbani dhidi ya Vita Club na Al Ahly kwa kupata ushindi hayo mawili yakifanyika kwa kiwango kikubwa, basi matumaini ya Simba kusonga mbele yatakuwa makubwa.
Mpaka sasa Al Ahly inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne itahitaji kupungfuza presha katika mchezo unaofuata baada ya huu wa Simba kwa kuhakikisha inashinda nyumbani kitu kitakacholazimisha maandailizi ya Simba yawe ya kina kirefu.
Nyuma ya Al Ahly kuna AS Vita yenye ponti tatu sawa na Simba ikiwazidi Wekundu wa Msimbazi kwa tofauti wa mabao ya kufunga. Wakongomani hao watabaki nyumbani wakiikaribisha JS Soura ya Algeria inayoshika mkia ikiwa na pointi moja.
Ili kuzidi kuikimbia Simba, AS Vita itahitaji kuendeleza ushindi wake ikiwa pale kwenye Uwanja wa Mashujaa jijini Kinshasa dhidi ya AJ Soura ambayo imeshamfukuza kocha wake Nabil Neghiz.
Katika toleo lijalo tutaendelea kuchambua zaidi juu ya silaha za Waarabu hao katika timu yao kwa undani kuhakikisha taarifa hizo zinawasaidia Simba.
MaoniMaoni Yako