Friday, January 25, 2019

PICHA - Kutana na Mama Mrembo Zaidi Duniani

Tags

Malezi ya mtoto huwa siyo kazi rahisi, ikiwa ni pamoja na kumuogesha, kumfulia, kumpa chakula na kuhakikisha afya nzuri na elimu bora ya mtoto. Hali hii ni ngumu zaidi kwa mzazi mmoja wa kike ambaye mzigo wa kifedha na malezi umo mikononi mwake. Machi 8 kila mwaka ni siku maalumu kuenzi juhudi za akina mama siyo tu katika malezi ya familia, bali pia katika jitihada zao kiuchumi. Makala haya yanaenzi nafasi adimu ya mama katika malezi.
Mimba za utotoni husababisha athari kwa mama na mtoto. Wasichana wadogo wanalazimika kukabiliana na shinikizo la kulea watoto peke yao na kuacha masomo wakiwa shule ya msingi, sekondari au chuoni. Bila elimu, hujikuta wakifanya kazi zenye ujira mdogo, ambao haukidhi mahitaji ya elimu bora kwa watoto wao. Pia, hukosa maarifa ya kuwa walezi bora, wabunifu wa fursa za kujikomboa kimaisha kwa sababu ya msongo wa mawazo unaotokana na changamoto nyingi za maisha zitokanazo na kutelekezewa jukumu la malezi na wazazi wenza.
Takwimu toka kituo cha huduma ya simu kwa mtoto (National Child Helpline) zinaonyesha mwaka jana pekee, zaidi ya asilimia 25 ya kesi zote zilizoshughulikiwa – zilihusu utelekezaji wa jukumu la malezi ya watoto kwa akina mama na mara nyingi akina mama hawa ama bado ni mabinti wadogo au hawana kipato cha kuwawezesha kutimiza mahitaji ya malezi kwa watoto.
Mfano, igizo la ‘Mwana Mpotevu’ linalorushwa redioni na Idhaa ya Ujerumani, DW. linafuatilia maisha ya wasichana wawili, Kassech na Askele, wote hawakupata elimu bora na bado wanaishi katika mtaa mmoja. Walipata mimba utotoni na sasa wana jukumu la kuwalea watoto wao. Kassech humkaripia na kumpiga mwanawe kinyume na mwenzake Askele, ambaye licha ya kuwa maskini, ni mama mwenye mapenzi kwa mtoto wake na hilo limemuwezesha mtoto huyo kufanya vyema shuleni. Mchezo huu unafuatilia kwa karibu maisha ya Kassech na jinsi anavyong’amua umuhimu wa kumpa malezi na elimu bora mtoto wake.
Kumbe akina Askele wapo wengi sana hapa kwetu, ambao hali zao na ‘uchanga’ wao haujawaondolea mapenzi kwa watoto wao.
Wasichana wanaojikuta katika uzazi wa mapema huwa katika hali halisi ya matatizo ya kifedha na maisha magumu wanayopitia akina mama hawa. Kama hii haitoshi, akina ‘baba’ wa watoto hawa ‘hukimbia’ majukumu kumuacha mama ahangaike. Ndiyo maana tukaandika makala haya kuuenzi mchango wa mama katika malezi ya mtoto. Nani kama mama?
Lakini mama naye kama binadamu huathirika na changamoto za kimazingira – mfano wa Kassech. Yawezekana kabisa msongo na ugumu wa maisha unachangia yeye kuwa mama anayemkaripia hata kumchapa mwanae mara kwa mara. Pia inaonyesha ni vipi mtoto anavyoweza kuathirika kwa kutokuwepo mzazi wa kiume. Hajui afanyeje wala kesho mtoto ale na avae nini. Huku jamii inayomzunguka ikimpa ‘jicho’ la kejeli kwa kulea/kuzaa mtoto nje ya ndoa.
Haya ni kati ya mengi wanayoyapitia akina mama siku hata siku. Hongereni kina mama. Ndiyo maana Waswahili waliona hili na kusema, ‘kuzaa si kazi – kazi kulea mwana.’ Haswa.
Nani manju wa malezi isipokuwa mama? Mama anabeba ujauzito kwa miezi tisa. Ananyonyesha kichanga chake kwa takribani miaka miwili. Awe ana fedha ama hana fedha, mtoto lazima anyonye. Ama kwa hakika mama ni mama tu.
Wito wetu ni kwa wanaume kote Tanzania, thamini mchango wa akina mama popote ulipo. Hasa pale ambapo unamuona mama akiwa katika hali ya uhitaji na wewe unao uwezo wa kumsaidia. Misaada hii si lazima iwe pesa. Hapana. Unaweza kumpisha mama/mjamzito katika kiti mkiwa safarini, kuomba kumsaidia kupakata kichanga chake na mambo kadha wa kadha. Inaanza na wewe