Mama Amuua Mtoto Kisa Wivu Wa Mapenzi Kwa Mumewe

  Mama Amuua Mtoto Kisa Wivu Wa Mapenzi Kwa Mumewe
MWANAMKE mkazi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kumkata na kisu shingoni mwanawe wa miezi sita, kutokana na ugomvi baina yake na mumewe kutokana na wivu wa kimapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara Augustino Senga akithibitisha kutokea kwa tukio hilo alisema tukio hilo limetokea Januari 20, mwaka huu, majira ya saa 12 jioni katika mtaa wa Kisimani kata ya Endiamtu wilaya ya Simanjiro mkoani humo.

Kwa mujibu wa Kamanda, Cecilia Paschal (29) mkulima na mkazi wa Mtaa wa Kisiwani, aligundulika kumuua mwanaye wa kumzaa, Frola Theophil kwa kumchinja na kumkata na kisu shingoni na baada ya kutenda tukio hilo alimeza dawa za hospitali ili aweze kujiua.

Chanzo cha tukio hilo, Kamanda Senga alibainisha kuwa ni wivu wa mapenzi kwani kabla ya tukio hilo inasemekana alikuta namba ya simu ya mwanamke iliyokuwa inampigia mume wake mara kwa mara.

Kutokana na hali hiyo, Januari 19, Cecilia na mumewe waliingia katika ugomvi mkubwa jambo lililosababisha mwanamume huyo kuondoka na kutorejea nyumbani kwake hadi baada ya kujulishwa tukio hilo.

“Taarifa zilitufikia mapema kutoka kwa majirani na watoto wake, Cecilia aliokolewa baada ya kukimbizwa katika Kituo cha Afya Mirerani. Kwa juhudi za madaktari alitapishwa na afya kurejea katika hali ya kawaida” amesema Senga.

Senga amekemea kitendo hicho kuwa ni kibaya na cha kusikitisha kwani mtoto huyo hakuwa na hatia na ameuawa kikatili kwa sababu ya mahusiano mabaya ya wazazi hao na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya wilaya kwa uchunguzi na kwamba mtuhumiwa ameshikiliwa na yupo kituo cha afya cha Mirerani akipatiwa matibabu.