Je? Wajua Siri Za Mashuka Ya Kigoma? Soma hapa na Ujionee maajabu

Mashuka yenye urembo wa maua ya kushonwa na rangi za kuvutia yameninginizwa pembezoni mwa barabara na nje ya nyumba kama uzio, ni ishara inayoweza kukujulisha kuwa umefika Kigoma.
Ni katika mji mkongwe wa Ujiji uliopo Kigoma Kaskazini, Magharibi mwa Tanzania eneo ambalo ni zaidi ya kilomita 1000 kutoka jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Waswahili wanasema usilolijua ni sawa na usiku wa giza, maana uwepo wa mashuka hayo si kwa ajili ya kujipatia kipato tu bali ni mila na desturi kama lilivyo vazi la khanga.
Na kuchagua mashuka mazuri, unahitaji usaidi wa kujua majina na ujumbe uliopo kwenye shuka unalolichagua.
Kila shuka lina jina lake, ambapo mengi yamebatizwa majina ya watu maarufu, wakiwemo viongozi wa kisiasa kama Mbunge wa mkoa huo Zitto Kabwe, Obama, Magufuli, Lowasa, Wema Sepetu na mengine mengi.
Huku majina mengine yakiwasilisha wanyama na vitu mbalimbali kama vile Pundamilia, Tausi, Nanasi, samaki wa kigoma, mwanamke mazingira, jumba la maneno, msala, pembe la ng'ombe, mwiba na kapu la kigoma.
Joslyn Anthon alianza kufuma tangu mwaka 1996 na anasema biashara hii inamfanya mwanamke ashughulike na kupata kipato.
"Huu ni utamaduni wetu kigoma , ukitafuta shuka za kufuma utazipata kigoma, Wanawake wa mkoa huu ni karibu wote wanajua kufuma mashuka haya na jambo muhimu kwao si kujipatia kipato tu bali ni kutunza mila na desturi yao."
"Mtu yeyote anayekuja anavutiwa na hayo maua ambayo wanayachora kwenye mashuka na ndio maana wanazianika nje ya nyumba zao na barabarani.
Shuka hizi zimeenea kimataifa, hata mgeni akija kigoma , ukumbusho mzuri kuwa aliwahi kufika katika mkoa huo ni shuka" Rafia aeleza.

Kivutio katika Mapenzi

Watumiaji wa mashuka haya wanasema sifa kubwa ya mashuka haya ni kudhihirisha upendo kwa mpenzi wako.
"Shuka hili likitandikwa huwa ni kivutio sana katika mapenzi, likitandikwa vizuri na kung'ara, nyumba inapendeza na lazima mtu aridhike"Lucy anaeleza.
Aliongeza kwa kutoa mfano kwamba kama ukinunua shuka la 'copy'ya Magufuli, hilo ndilo la kisasa zaidi na gharama yake kubwa hivyo hata ukitandika kumuandalia mume wako anaona kuwa kweli ameandaliwa.
Ni chapa mpya hivyo mpenzi wako anajihisi kuwa yeye ni mpya siku zote.
"Leo nimetandika hilo shuka kwa alama ya upendo na hivyo hata mume wako anaweza kujisikia faraja kuwa mke wangu ananipenda, kuna mashuka mengine yana maandishi mfano nilikuwa na shuka lililoandikwa mahaba ya dhati, nililiuza gharama kubwa sana" Lucy asisitiza.
Huku Zainab Karabona anasema pamoja na kuwa wengi wanafuma kwa ajili ya matumizi na biashara lakini lengo kubwa ni kupendezesha chumba hata mtu akiingia ndani aseme mashallah na huwa wanatua zawadi ili kuonyesha upendo.

Ubunifu wa maua

Uwesu Bin Amour ni mchoraji na mbunifu wa maua haya ya mashuka ,yeye aliweza kujifunza kwa kipindi cha wiki tatu kupata ujuzi huo.
Anasema kila mchoraji ana namna yake ya kuchora hivyo hata akichora na shuka likawa limefumwa anajua kuwa ni kazi yake.
"Hata nikipita mkoani nikaliona shuka ambalo nilichora mchoro wake ninakuwa ninajua kuwa ile ni 'art' yangu," Uwesu aeleza.
Bwana, Uwesu anasema wao huwa huwa wanachora maua hayo kutokana na umaarufu wa mtu.
"Kuna wakati wateja wanakuja na kutaka mtindo anaotaka au anaweza kunipa uhuru wa kuchora mchoro wowote.
Huwa tunaangalia umaarufu wa mtu kutokana na soko,kwa mfano Zitto Kabwe ana umaarufu hivyo hata mashuka yake huwa yananunuliwa kwa wingi.
Au mtu anaweza kuja anataka kuchorewa copy ya Wema Sepetu hivyo nnakuwa najua anataka mfumo wa mjazo" Mchoraji Uwesu afafanua.
Aidha fani hii anadai kuwa inawasaidia vijana kupata kipato, gharama ya mchoraji utegemea na jina la shuka , kama mchoro wa copy ya Magufuli au ndege tausi ni shilingi 4000 mpaka 5000 ambapo ni sawa na dola mbili.
Huku mchoro wa Lowasa ,Obama na mingine mingi huwa zinachorwa huwa ni dola moja.

Siri ya ufanisi wao


Esha Ali ana zaidi ya miaka 10 anafuma mashuka katika ufumaji wa mashuka. Yeye anapenda kutengeneza shuka aina ya makunguru, mjazo, mnyororo na mwiba.
Anasema vigezo ambavyo mtu anapaswa kuviangalia unaponunua shuka ni kuangalia Ua,ubora wa shuka, ufumaji , aina ya kitambaa ambacho kimetumika.
Majina ya mashuka huwa yanarahisisha kazi kati ya mfumaji, mchoraji na mteja.
"Unahitaji kuwa na ujuzi maana ukikosea kidogo tu , unakuwa unakosea kila kitu.
Mfano unaweza kujua ufumaji wangu na mtu mwingine kwa upande wa ubora unaweza usilingane.
Kuna wale ambao unakuta anafuma makunguru ambayo yanatoa chongo na mchoro unakuwa haupendezi kwenye shuka.
Mfumaji anatakiwa kufuata mchoro ulivyo ili kuweka ubora wa shuka" Bi.Esha.
Mara nyingi mifumo huwa inategemea na mtu mwenyewe, mfano shuka la Lowasa lina minyororo mingi na majina huwa yanatolewa kulingana na sifa za huyo kiongozi au mtu.
Mfano kama copy ya Magufuli ziko aina tofauti tofauti, na huwa zinabuniwa kulingana na kila anachokifanya Magufuli kinakuwa kinawakilishwa kwenye shuka.
Kuna shuka la Zitto ambalo halina maua katikati ila kuna maua pembeni.
Ubora ndio sifa ambayo wateja wengi wamekuwa wakiyapenda kwa sababu huwa hayachaniki kwa haraka na rangi zake zinavutia.
Kwa sasa mashuka haya yanasafirishwa kuuzwa maeneo tofauti tofauti hata ulaya.
Kufuma ni sawasawa na kusuka ukili kuna ambao wana mkono mzito na wengine wako wepesi, hivyo kuna ambao wanaweza kuchukua wiki ,mbili au mwezi na wengine hata miezi mitatu.

Changamoto zinazowakabili

Bei ya kuuza mashuka hayo bado ni ndogo ukilinganisha na muda ambao wanautumia ndio maana unakuta mfumaji mashuka hategemei biashara hiyo tu bali anakuwa anafanya na shughuli nyingine.
Gharama za shuka zinaanza kwenye shilingi 35,000 - 150,000 za Tanzania.
Mauzo huwa yanategemea msimu na huwa inategemea muda wa mfumaji.
Aziza Abedi yeye anauza sabuni ambazo anazitengeneza mwenyewe , na akiwa sokoni anakuwa anafuma mashuka yake.
Pamoja na ustadi wa kazi yao kwa enzi na enzi, lakini sasa kilio chao ni upatikanaji wa teknolojia.
Bi. Khadija Mgamba ambaye anatumia mashuka yake kupamba harusini.
"Biashara hii ya kuuza mashuka yaliyofumwa maua ya urembo kwa mkono,hivi sasa yamekuwa na kuwa mchango mkubwa sana kwa maeneo hayo na hata unaweza kukuta familia nzima ,baba ,mama na watoto wanafuma.
Licha ya kuwa wanawake ndio wafumaji wakubwa.
Yeye anadhani kwamba, wakipata mashine basi kazi itakuwa rahisi zaidi na wataweza kutengeneza maua mazuri kwa wingi" Bi.Mgamba asisitiza.


MaoniMaoni Yako