Chatu Aokolewa Baada ya Kuzidiwa Nguvu na Kupe Nchini Australia

Wakamata nyoka nchini Australia wamemnusuru chatu ambaye alikuwa amevamiwa na mamia ya kupe.
Chatu Aokolewa Baada ya Kuzidiwa Nguvu na Kupe Nchini Australia
Mnyama huyo ambaye alikuwa mgonjwa alifunikwa kabisa na kupe hao, na alikutwa ndani ya bwawa la kuogelea katika eneo la Gold Coast jimboni Queensland.
Mtaalamu wa kunasa nyoka alimtoa nyoka huyo kwenye bwawa na kumkimbiza katika hospitali ya wanyama kwa matibabu.
Madaktari wa wanyama waliondoa kupe zaidi ya 500 kutoka kwenye mwili wa nyoka huyo. Tony Harrison, ambaye ndiye alimnusuru nyoka huyo ameiambia BBC kuwa inatarajiwa nyoka huyo atapona kabisa.
Chatu Aokolewa Baada ya Kuzidiwa Nguvu na Kupe Nchini Australia
Bw Harrison anaamini kuwa nyoka huyo alikuwa akijaribu kuwazamisha kupe hao kwenye maji ili ajinusuru.
"Bila shaka [chatu huyo] hakuwa na raha kabisa," amesema.
"Uso wake wote ulikuwa umevimba na ulikuwa umefunikwa na kupe waliokuwa wakimnyonya."
Amesema kumyanyua nyoka huyo ilikuwa ni kama "kubeba begi la marumaru ambazo zilikuwa zikitembea kwenye mkono wangu".
Nyoka kwa kawaida huvamiwa na kiasi kidogo cha kupe na wadudu wengine mwituni, amesema Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Queensland.
Hata hivyo, mtaalamu huyo anasema kuvamiwa na kundi kubwa la wadudu hao inaashiria kuwa nyoka huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi yaliyotokana na joto kali ama ukame.
"Ni dhahiri kuwa alikuwa anaumwa mpaka akashindwa kujilinda kabisa. Sidhani kama angelipona iwapo asingeliokolewa na kupelekwa kupatiwa matibabu," Profesa Fry ameeleza.
Mwokozi wake, Bw Harrison baadae akaeleza kuwa nyoka huyo aliyepewa jina la Nike alipata maambukizi japo sasa "anaendelea vyema".
"Nike leo kiasi amekuwa mchangamfu," amesema Bw Harrison katika video iliyopakiwa kwenye ukurasa wa Facebook wa wakamata nyoka wa Gold Coast na Brisbane .
"[Hata hivyo] ataendelea kulazwa kwa muda mrefu kidogo [katika kitua cha uhifadhi na matibabu ya wanyama cha Currumbin Wildlife Sanctuary] mpaka hali yake itakapotengemaa na kurudishwa mwituni."

MaoniMaoni Yako