Muandaaji wa mashindano ya ulimbwende ya Miss Tanzania Basila Mwanukuzi ameiambia BBC kuwa wale wote wanaotoa kasoro mashindano ya mwaka huu, wanachuki na hawapendi maendeleo.
Bi Mwanukuzi kupitia kampuni yake The Look ameandaa mashindano hayo kwa mara kwanza mwaka huu. Mashindano hayo yamekuwa yakiyumba kwa miaka kadhaa lakini mwaka huu kumekuwa na mwamko wa kipekee.
Kilele cha mashindano hayo kilikuwa siku ya Jumamosi ambapo mlimbwende Queenelizabeth Makune aliibuka mshindi. Pamoja na vitu vingine, mlimbwende huyo alizawadiwa gari na waandaaji wa shindano hilo.
Hatahivyo, wakosoaji mitandaoni walikashifu ubora wa zawadi hiyo wakisema haiendani na hadhi ya mashindano hayo. Baadhi ya wakosoaji walienda mbali zaidi na kusema mashindano hayo hayakupendeza.
Akiongea na BBC Bi. Mwanukuzi ambaye pia ni mshindi wa mashindano hayo mwaka 1998 amesema licha ya changamoto zilizokuwepo malengo yake ni kuendelea kupeperusha bendera ya Miss Tanzania.
"Haya mashindalo licha ya kwamba yalikuwa yameshuka, watu wengi walikuwa wanayataka kwa sababu ni brand ya taifa.
Ni kitu kikubwa sana. Kwa mtizamo wa kibiashara ni kitu kizuri kama ambavyo ilivyo Miss World na mashindano mengine," amesema Bi Mwanukuzi na kuongeza: "Mimi nimepata baraka zote za serikali watu, wanaona hii ni brand kwahiyo usifikiri kwamba hata kama mambo yameenda vizuri sana kila kitu kitasifiwa, Hapana.
Na chapili mashindano tumefanya katika kipindi kigumu ambacho kilikuwa hakuna sponsorship (udhamini) kwa hiyo karibu kila kitu nimegharamikia mwenyewe."
Bi Mwanukuzi amesema picha ambazo zimesambazwa mitandaoni zinazoonesha gari la zawadi likiwa limechakaa ni za kutengeneza "... watu hao hao ambao wanachuki ndio wanachukua picha (za zawadi ya gari) na kuzi edit (hariri) na kusambaza mitandaoni...mtu akiona na kinaonekana cha kwa kweli siyo rahisi (kutoamini) hadi aone ile zawadi nyengine.
Lakini nashukuru watu waliokuwepo na walioona live (mbashara) ndio hao hao wanaonitetea huko mitandaoni kuonesha kitu hiki si sawa na kitu halisi ni hiki hapa," amesema Bi Mwanukuzi.
Miongoni mwa kasoro kubwa zilizokuwa zikiiandama Miss Tanzania ni kashfa za upendeleo na ufuska baina ya washiriki na waandaaji, kwa mwaka huu Bi Mwanukuzi amesema hayo hayakujitokeza, "Wanataka kuonesha kuwa mashindano hayajafanikiwa lakini yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, hatujasikia malalamiko ambayo tulikuwa tunasikia huko nyuma ufuska sijui vitu kama hivyo havijasikika hata kidogo.
Hatujasikia malalamiko ya upendeleo hata kidogo, warembo walikuwa katika viwango vya hali ya juu kwasababu waliniamini na wakajitokeza."
Kuhusu changamoto ya udhamini, Bi Mwanukuzi anaamini mwakani watajitokeza kwa wingi na kusema kuandaa mashindano hayo na kuyarudisha kwenye umaarufu wake wa awali ni fursa muhimu kwake na kwa walimbwende wengine wanaohitaji fursa hiyo.
"Kwa kutambua umuhimu wa mashindano haya na jinsi yalivyo kua katika hali ile nikaona hapana. Hii ni fursa ya warembo ni fursa ya vijana wakike wa mikoa yote nchi nzima.
Sisi wote tulitoka huko tunaorodha ya warembo ambapo tunaona mambo makubwa wanayoyafanya kwasababu walipita kwenye Miss Tanzania.
Kwa hiyo haikuwa jambo zuri kitu kikubwa cha kitaifa kama hicho kiishie hivyo hivyo tu. Kwahiyo nikajitolea ni kama wito japo pia ni biashara, lakini ni kazi kubwa sana."
MaoniMaoni Yako