Lungi Amkingia Kifua Zari Amuwashia Moto Gigy Money

Lungi Amkingia Kifua Zari Amuwashia Moto Gigy Money
Mwigizaji mkongwe wa filamu Bongo, Lungi Maulanga amemwashia moto msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Gift Stanford ‘Gigy Money’, kisa mjasiriamali maarufu Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady.’

Akizungumza na Ijumaa, Lungi alisema amekuwa akikerwa mno na Gigy ambaye amekuwa akitoa kauli ya kuwa yeye ni mzuri na mrembo kuliko Zari, jambo ambalo siyo kweli kwani msanii huyo hawezi kumfikia hata robo mwanamama huyo ambaye ni raia wa Uganda mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini.

Lungi aliendelea kumtemea cheche Gigy kwamba kwa jinsi alivyo alitakiwa kuwa mtunza bustani nyumbani kwa Zari na siyo vinginevyo. “Huyo Gigy alipata jina kwa kukaa utupu, lakini Zari ni mwanamke mpambanaji na ana pesa zake siyo anadanga, sasa namshangaa huyo mtoto kujilinganisha naye.

“Ni bora hata mimi nikajilinganisha naye kwa sababu hapa nina watoto wanne, lakini bado ninaonekana mrembo. “Sina hata tumbo, lakini yeye mtoto mmoja tu utadhani anao zaidi ya watano, namsihi anyamaze na aache kutafuta kiki kupitia jina la Zari maana siyo levo zake,” alisema Lungi.

Ili kuleta usawa wa habari hii, Ijumaa lilimtafuta Gigy kwa njia ya simu yake ya mkononi, lakini iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa meseji na kuulizwa anazungumziaje kauli ya Lungi hakujibu chochote hadi gazeti hili linakwenda mitamboni. Hivi karibuni Gigy alinukuliwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari akisema kwamba yeye anamzidi mwanamama Zari kwa uzuri, kauli ambayo ilizua gumzo kubwa.