Yanga ikifanya hivi mbona safi tu

Dar es Salaam. Waswahili wanasema unapojikwaa usiangalia ulipoangukia bali ulipojijwa ndicho kinachotakiwa kufanywa na Yanga kwa sasa katika dirisha hili la usajili.
Yanga ikiwa katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika imekuwa na matokeo mabaya katika mashindano yake mbalimbali katika msimu huu.
Hata hivyo; tovuti ya Mwanaspoti imeangalia maeneo matatu ambayo uongozi wa Yanga ukifanyia kazi timu hiyo inaweza kurudi katika ubora wake.
Katika kipindi hiki cha usajili klabu hii inatakiwa ipate wachezaji imara ambao wanaweza kuongeza nguvu, ili kuimarisha kikosi chao kwaajili ya msimu ujao pamoja na Mashindano ambayo wanashiriki.
KIPA WA KULETA CHANGAMOTO
Mashabiki wa Yanga wamekuwa hawana imani na kipa wao Youthe Rostand kutoka na kiwango duni alichokionyesha msimu huu.
Kukosekana kwa Beno Kakolanya baada ya kusumbuliwa na majeraha ya goti, Yanga walikuwa wakilazimika kumtumia kipa wao chipukizi, Ramadhan Kabwili, hali ambayo ilikuwa changamoto kwao.
Kuna tetesi ndani ya klabu hiyo kwamba wapo mbioni kuachana na Rostand, lakini wanatakiwa wahakikishe kwamba wanapata kipa mwingine ambaye anakuja kuleta ushindani ndani ya kikosi hicho.
Vile vile pia wanatakiwa kuwa makini kwani Kakolanya inasemekana anawachungulia kwa jicho la pembeni, kwani tayari ana ofa uhakika ndani ya kikosi cha JKT Ruvu.
BEKI WA KATI
Katika upande wa beki ya kati, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondani pamoja na Nadir Haroub, lakini mara kwa mara katika nafasi hiyo, imezoeleka kuchezwa na Yondani pamoja na Dante.
Ninja na Nadir wameonekana kuwa chaguo la pili katika kikosi hicho, huku Ninja akionekana kabisa ajawa mchezaji mwenye utulivu, huku Nadir umri ukionekana kuanza mkumtupa mkono.
Kikosi hicho kimekuwa kikihaha sana pindi Yondani na Dante wanapokeosekana, hivyo huu ndio wakati sahihi ambao wanaweza wakapata mibadala ya Yondani na Dante.
Yanga wanatakiwa wapate beki kisiki kama Nurdin Chona (Prison), kwani ni mchezaji mwenye nguvu na akili na amekuwa na msaada mkubwa katika kikosi cha Prison, hivyo ni jukumu la kamati ya usajili katika klabu hiyo kuhakikisha wanapata mtu wa kazi katika eneo la kati.
KIUNGO MCHEZESHAJI
Zile kampa kampa tena zimepotea kabisa ndani ya duara la katikati katika kikosi cha Yanga. Viungo kama Thabaan Kamusoko na Papy Tshishimbi.
Yanga inahitaji aina ya kiungo kama Mohammed Ibrahim au Hassan Dilunga katika eneo hilo la kiungo kwani ni wachezaji ambao wanajua kunyambulika na kupiga pasi za mwisho.
Mohammed Ibrahim anaweza akawa chaguo muhimu hivi sasa kutokana na kukosa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba, lakini vile vile Dilunga ni mtu ambaye ameshapita katika kikosi hicho hivyo falsafa anazielewa.
Chipukizi Maka Edward ni mchezaji anayetumia nguvu katika kukaba, kupiga mipira mirefu ‘High Ball’ kuliko pasi za chini chini ‘Short Pass’, ambazo mtu kama Haroun Niyonzima alikuwa akipiga.
Yanga bila kuficha wanahitaji kiungo wa kunyambulika ambaye nyuma yake wanakuwa wanacheza Thaban Kamusoko pamoja Papy Tshishimbi.
STRAIKA MPAMBANAJI
Kukosekana kwa Donald Ngoma bila kupepesa macho ni kwamba kulichangia kikosi hicho kuyumba msimu huu, lakini hata kwa upande wa Amis Tambwe nalo lilikuwa pigo jingine.
Wachezaji hawa wakikaa pale mbele walikuwa na uwezo mkubwa wa kufanya lolote kwani Ngoma alikuwa na nguvu ambapo Tambwe yeye alikuwa na kazi moja tu ya kutupia mipira wavuni.
Azam kwa kutambua hilo wakamsajili Ngoma kwani kuondoka kwa John Bocco katika kikosi chao walijikuta wamekosa mchezaji wa upambanaji kwahiyo wao wenyewe wameshtuka kwamba wanahitaji mpambanaji.
Kwa upande wa Yanga ambao mpaka hivi sasa wamekaa kimya, wanahitaji aina ya Ngoma kutua katika kikosi chao, kwa haraka haraka naweza kusema wanahitaji mchezaji kama Ditram Nchimbi kwani ana nguvu nyingi pia ni mpambanaji.