Monday, June 11, 2018

Wizi wa kampuni za simu kwa wateja mwisho

 

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezindua mtambo wa kisasa wa kudhibiti matumizi ya huduma za mawasiliano kwa kampuni za simu na watumiaji ambao utawezesha wenye simu kutokatwa malipo ya ziada na kijanja janja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, baada ya kukagua mtambo huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa alisema mtambo huo utawezesha kuangalia simu zinazotoka na kuingia kwenda mitandao mingine na gharama zinazotozwa.
Aidha, alisema Mbarawa, mtambo huo pia utawezesha makusanyo sahihi yanayokusanywa na kampuni za simu na kuonyesha matumizi ya fedha zinazotumiwa na kampuni za simu kwa huduma zinazotoa.
"Mtambo huu utaangalia ulaghai unaofanywa na kampuni za simu, miamala ya pesa inayotumwa na kuingia kwenye simu, simu zinazoingia na kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha tunakusanya mapato sahihi," alisema Prof. Mbarawa.
Alifafanua zaidi kuwa serikali imeamua kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano ambayo inakua kwa kasi ili kuhakikisha wapata huduma wananufaika.
Waziri Mbarawa alisema mfumo huo wa kisasa utawezesha kuona kila kitu kinachofanywa na mitandao ya simu kwa upande wa fedha.
Alisema pia kuna mfumo wa kuangalia madhumuni yanayofanywa na kampuni za simu na mfumo wa kuangalia mapato kwenye serikali kuanzia ngazi ya halmashauri.
Kumekuwapo na malalamiko ya muda mrefu ya wateja wa kampuni za simu kukuta salio lao la fedha, vifurushi ama data limekwisha baada ya matumzi ya muda mfupi, katika mazingira ya ajabu.
Lakini Prof. Mbarawa alisema: "Naomba nichukue nafasi hii kuwaeleza Watanzania kuwa huduma zitakazokuwa zinatolewa na simu zitakuwa sahihi, wapige simu kwa wingi kwa sababu wako salama na pia usalama wa fedha wanazotumia unahakikiwa."
Aidha, waziri huyo aliwataka watumiaji wa mitandao kutotumia sekta ya mawasiliano kufanya uhalifu wa aina yoyote kwa sababu kuna mitambo ya kisasa ya kuwabaini.
Pia alisema TCRA imejipanga kubadili mifumo na mitambo wanayotumia kulinda usalama wa watumiaji ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia za wezi wa mitandaoni.
"Tutajitahidi kuwa mbele mara mbili zaidi kwenye teknolojia zetu za kudhibiti wahalifu ili kukabiliana na mbinu zinazotumiwa na wahalifu mara kwa mara," alisema Prof. Mbarawa.
Alisema kwa sasa sekta hiyo ina wateja wa simu takribani milioni 40.5 na watumiaji wa intaneti milioni 23.
Aidha, Prof. Mbarawa alisema watumiaji wa fedha kwa simu ni milioni 22 na kwamba hadi kufikia Disemba mwaka jana kiasi cha fedha zilizotumwa mitandaoni ni takribani Sh. trilioni 103.
Naye Mtafiti Mwandamizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa TCRA, Emmanuel Manasseh, alisema mtambo huo una kazi ya kuhakiki mapato ya watoa huduma.
Alisema pia mtambo huo unakusanya taarifa zote za wanaoongeza salio kwa kutumia kadi za kukwangua, elektroniki, mawakala na kukusanya taarifa zote za kutumia huduma za mawasiliano.
"Pia gharama za wanaotumia kupiga simu za ndani ya nchi na nje, kutoka nje ya nchi kuja nchini na wale wanaoingia nchini na kutumia mitandao ya simu za Tanzania na gharama zinazohusika," alisema.
Alisema mtambo huo pia unaangalia simu zinazoingia na kutoka zinakuwa kwenye mfumo sahihi na kubaini zile zinazozuiliwa na mitandao ya simu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, James Kilaba, alisema pia wanachunguza wezi mitandaoni wakiwamo wanaoomba fedha kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno na kwamba uchunguzi utakapokamilika watatangazwa hadharani.
Mhandisi Kilaba alisema wamepokea malalamiko ya watu kuombwa fedha na watu wenye namba zilizosajiliwa na kampuni za simu na kusema kuwa ni kinyume cha sheria ya usalama mitandaoni.
"TCRA inaendelea kufanyia kazi suala hili ili kuhakikisha usalama wa watumiajia wa mitandao ya simu, tunachunguza pindi tutakapokamilisha uchunguzi wetu tutawatangaza wahalifu hadharani," alisema.
Mhandisi Kilaba alisema pia wanatoa elimu kwa jamii kupuuza ujumbe wa aina hiyo na wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua zichukuliwe dhidi yao.

No comments:
Write comments

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();

Facebook