"Yanga tulieni nakuja" Marcellin

MSHAMBULIAJI wa Benin na klabu ya Buffles du Borgou FC, Marcellin Degnon Koukpo ambaye amedaiwa kutua nchini na kusaini mkataba wa kujiunga na Yanga, amekanusha taarifa hizo na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani kutulia.

Koukpo ambaye amekuwa akifukuziwa na Yanga kwa msimu wa tatu huu, ameliambia BINGWA kwa njia ya simu akisema hajasaini mkataba wowote na klabu hiyo na wala hayupo nchini Kenya.

“Mimi bado niko huku Benin, lakini naomba mashabiki wa Yanga watulie, mazungumzo yanakwenda vizuri, tukishamalizana nasubiria tiketi nakuja Tanzania,” alisema mshambuliaji huyo kipenzi cha mashabiki wa soka Benin.

Chanzo kimoja cha karibu na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/2017, kimesema Yanga walitaka kumleta nyota huyo wa timu ya Taifa ya Benin kwa ajili ya kufanya majaribio, lakini alikataa na kuamua kufanya naye mazungumzo ya kumsajili.

“Koukpo hajasaini Yanga, hajaja nchini Tanzania wala hayupo Kenya, tatizo ni kwamba Yanga walitaka aje kufanya majaribio akakataa, lakini mazungumzo yamefanyika na kwenda vizuri,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa mchezaji huyo huenda akatua nchini Jumatano hii na kumalizana na klabu hiyo ya Jangwani.