Pochettino, Low wanukia Madrid

ZINEDINE Zidane amechukua uamuzi wa kustusha wa kutangaza kujiuzulu kuwafundisha, Real Madrid ikiwa ni siku chache tangu awasaidie  vigogo hao wa Hispania kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari aliouitisha ndani ya muda mfupi jana, Mfaransa huyo mwenye miaka 45 alithibitisha kujiuzulu nafasi yake ya kuifundisha Madrid baada ya Jumamosi kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Liverpool jijini Kiev na kuwa kocha wa kwanza kushinda taji hilo la Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo.
"Huu ulikuwa ni muda sahihi mimi kuondoka, tumeshashinda mataji yote pamoja, nitaanzaje kuwaomba wachezaji wafanye zaidi ya waliyofanya. Wanahitaji kusikia sauti mpya, kocha mpya, atawapa motisha na mbini mpya," alisema Zidane.
Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, akizungumza mapema katika mkutano huo alisema: "Ni siku ya huzuni, kwangu, timu, wachezaji na kila mmoja wetu kwenye klabu hiiI. Ni uamuzi ambao hatukuutarajia, nilimpenda akiwa mchezaji, na kocha, na nilitaka kuona kila siku anakuwa katika upande wangu. Lakini pale anapoamua kufanya uamuzi, kitu pekee ambacho tunaweza kukifanya ni kuuheshimu.
"Nimechukua muda mrefu kumshawishi, lakini ninamjua vizuri ni mtu wa aina gani na kitu kingine ninachoweza kukifanya ni kumpa heshima na kutambua mchango wake, na kumweleza anakaribishwa muda wowote kuja hapa ni nyumbani kwake.
"Hii ni mpaka pale ambapo sina shaka kuwa atarejea tena.Ingawa kama unahitaji mapumziko, tutamwelewa. "Januari mwaka 2016, Zidane (45), alijiuzulu katika nafasi yake akiwa kocha wa vijana wa Castilla, na akiwa amemaliza msimu kwa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati pia alichukua kombe la La Liga msimu wa 2016-17 pamoja na mataji mawili ya Klabu Bingwa Dunia, mawili ya Kombe la UEFA na Kombe la Hispania.
Mfaransa huyo alionekana kwenye kipindi kigumu katikati ya msimu wa 2017/18, baada ya Madrid ikiwa nyumbani kufungwa mabao 3-0 katika mechi ya El Clasico na kuwapa nafasi Barcelona ya kujiimarisha kwenye mbio za kutwaa taji la La Liga, na timu hiyo maarufu Los Blancos kutolewa kwenye mashindano ya Kombe la Copa del Rey na Leganes kwenye Uwanja wa Bernabeu.
Kuwa na mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwafunga mahasimu wake Paris Saint-Germain, Juventus na Bayern Munich na Jumamosi kuifunga Liverpool jijini Kiev --na kuiweka Madrid kwenye rekodi ya kushinda taji hilo mara nyingi zaidi, mara ya 13, ilionekana kama Mfaransa huyo ataendelea na kibarua chake ndani ya klabu hiyo, na kila siku Perez alionekana kumtetea kocha huyo hadharani.
Tofauti kati ya kocha huyo na Perez zilianza kuonekana kwa kutokubaliana kumsajili kipa chipukizi wa Athletic Bilbao, Kepa Arrizabalaga, ambapo Zidane kwa upande wake alisema anafahamu nafasi ya kuifundisha Madrid si ya muda mrefu na anajua huenda majira ya kipindi cha joto kutakuwa na mabadiliko.
Upepo sasa unageukia kwa nani anayefaa kurithi mikoba ya Zidane, na makocha wawili wanaopewa nafasi ni  Mauricio Pochettino wa Tottenham na Joachim Low anayeifundisha timu ya Taifa ya Ujerumani, ambao wote hivi karibuni wamesaini mikataba mipya ya kuziongoza timu zao.
Mwaka 2006, Zidane pia alitangaza uamuzi wa kustaafu kuitumikia Real Madrid kwa kustukiza, wakati huo akiwa na miaka 33 baada ya mechi ya fainali ya Kombe la Dunia licha ya kuwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na klabu hiyo.
MaoniMaoni Yako