Paolo Guerrero: Aliyetetewa na wapinzani aruhusiwa kucheza Kombe la Dunia.

Nahodha wa Peru Paolo Guerrero anaweza kucheza kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi, jopo la mahakama nchini uswizi limeamua.

Mahakama hiyo ilikubaliana kuondoa kwa muda marufuku ya kutocheza miezi 14 ambayo ilikuwa imetolewa dhidi ya mchezaji huyo na Mahakama ya kutatua Mizozo ya michezo (CAS).
Mahakama hiyo ilichukua hatua hiyo huku ikiendelea kusikiza rufaa ya mshambuliaji huyo wa miaka 34.

Manahodha wa timu zilizopangwa kucheza na Peru katika Kundi C Australia, Denmark na Ufaransa walikuwa wameliandikia barua Shirikisho la Soka Dunia Fifa kuwataka wamruhusu mchezaji huyo kucheza.

Guerrero, ambaye alipatikana na kosa la kutumia kokeni Oktoba, anasema alijipata amekunywa dawa hizo akinywa chai.
Anatumikia marufuku ya miezi 14.

Kupitia barua kwa Fifa, manahodha hao watatu waliomba kuwe na "kusitishwa kwa muda" kwa marufuku yake ndipo aweze kuchezea Peru nchini Urusi.

Kokeni kwenye chai.

Guerrero, 34, alipatikana ametumia kokeini wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Argentina mnamo 6 Oktoba na akapigwa marufuku ya miezi 12 awali.

Marufuku yake ilipunguzwa hadi miezi sita na kamati ya rufaa ya Fifa lakini shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa zilizoharamishwa michezoni (Wada) lilikakata rufaa uamuzi huo kwenye Mahakama ya Mizozo ya Kimichezo (Cas) ambayo ilimpiga marufuku ya miezi 14.

Mahakama nchini uswizi sasa imeamua kuwa hatua ya kuongeza marufuku hiyo haikuwa ya haki na imeondoa utekelezwaji wa marufuku hiyo kwa sasa, hatiua inayomwezesha Guerrero kucheza katika michuano hiyo itakayoanza mnamo 14 Juni nchini Urusi.

Peru walilaza New Zealand kwenye mechi mbili za muondoano wa kufuzu Novemba ndipo wakafuzu kwa Kombe la Dunia.
Itakuwa mara yao ya kwanza kushiriki tangu mwaka 1982.