Monday, June 11, 2018

Mzee Rashid alivyoibuka shujaa mbele ya Magufuli

 

MJUMBE wa nyumba kumi katika eneo la Kinondoni Shamba jijini Dar es Salaam, Rashidi Mashaushi, jana aliamka na bahati ya pekee baada ya kujikuta akizungumza ana kwa ana na Rais John Magufuli ambaye alimpatia Sh. 200,000, alipowasilisha kero ya mafuriko katika eneo lake.
Mashaushi aliikwaa bahati hiyo baada ya kuzungumza na Rais Magufuli aliyekuwa ametoka kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti mkuu wa Bakwata unaojengwa kwa ufadhili wa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI.
Msikiti huo ambao unatarajiwa kukamilika Aprili, mwakani unajengwa katika kiwanja zilizopo ofisi za Baraza Kuu la Waislamu, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mara baada ya kutoka kwenye uzio wa kiwanja cha Bakwata, Rais Magufuli alisimama kwenye gari lake na kuwaeleza wananchi kilichompeleka eneo hilo na kisha kutaka wananchi waliokuwepo wamueleze kero zao.
Mashaushi alipopewa kipaza sauti alisema kwamba kwenye eneo wanaloishi wamekuwa wakisumbuliwa na mafuriko mara kwa mara hivyo wanajitaji kuboresha miundombinu.
Alisema anaishi Kinondoni Shamba na kwamba msikiti huo utakuwa ni jirani na wakazi wa eneo lake lakini kuna sehemu ndogo ambayo husababisha mafuriko kwa wakazi wa eneo hilo na pia ubovu wa barabara.
"Kuna kakipande kadogo ka mfereji kanatusumbua maji yanatuama sana Kinondoni Shamba... nikiangalia kwa upande mwingine Mheshimiwa Rais wetu alikuwa jirani yetu hapo Leaders na mimi ni mjumbe wa nyumba kumi CCM, hii ndiyo changamoto ya wakazi wa Kinondoni Shamba," alisema.
Mashaushi alisema kuna wakati Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, alikwenda hapo na kuwawezesha kidogo lakini mambo bado hayajakaa vizuri hadi sasa.
"Tunaomba umuombe Mfalme wa Morocco angalau atuwezeshe kama utatuombea ombea tubomolewe baadhi ya nyumba mambo yawe shwari, waje wafadhili watusaidie. Kwa kweli sisi tunajua kwamba tukisubiri ruzuku Serikali Kuu itakuwa mtihani kidogo kibajeti," alisema.
Baada ya mzee Mashaushi kusema hayo, Rais Magufuli alitaka kujua eneo hilo lenye tatizo lina urefu wa kilomita ngapi.
Mzee Mashaushi alimjibu Rais Magufuli kuwa kipande hicho siyo kikubwa kwa kuunganisha hadi Uwanja wa Biafra (umbali wa kilometa mbili).
Rais Magufuli alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitatue suala hilo kuanzia siku ya jana na kumwagiza kuchukua namba ya simu ya mzee huyo.
"Nakushukuru sana kwa sababu umezungumza kwa niaba ya wananchi... hongera sana, Mkuu wa Mkoa chukua namba ya simu ya Mashaushi kama ni vocha nitakuongezea, chukua namba yake uje utembelee eneo hili na kama ni kazi ianze mara moja," alisema.
Aidha, Rais Magufuli aliagiza zichukuliwe fedha za Mfuko wa Barabara za Manispaa ya Kinondoni ili zitumike kutengeneza barabara hiyo iliyotajwa na Mashawishi.
"Ninaagiza kuanzia leo (jana) barabara hii ianze kutengenezwa kwa kutumia fedha hizo kwa heshima ya mjumbe wa nyumba kumi wa CCM, na hiyo barabara iitwe kwa jina lake 'Rashid Road'," alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alimkabidhi mzee Mashaushi Sh. 200,000 huku akimweleza kuwa anapenda watu wa namna hiyo.

No comments:
Write comments

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();

Facebook