Mtibwa Sugar mabingwa wapya Kombe FA


Arusha. Mtibwa Sugar imetwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa kuichapa Singida United mabao 3-2 katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Ushindi huo unaifanya Mtibwa Sugar kukata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hiyo itategemea uamuzi wa CAF.
Kumekuwa na 'sintofahamu' kwa Mtibwa Sugar ambao mwaka 2004 walipewa adhabu na CAF baada ya kushindwa kwenda kucheza mechi yao ya ugenini dhidi ya Santos ya Afrika Kusini wakafungiwa miaka mitatu.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema: "Bingwa wa mashindano haya ndiye ataiwakilisha nchi kwenye michuano hiyo na tutapeleka jina lake. Mengine tunasubiri uamuzi ya CAF."
Katika mchezo huo Mtibwa Sugar ilianza kwa kasi na kutawala mchezo huo na shujaa wao alikuwa Ismail Mhesa aliyefunga bao tatu na ushindi katika dakika ya 88 akiunganisha pasi ya Kelvin Sabato.
Mtibwa walilazimika kuwa pungufu katika dakika hizo baada ya Issa Rashid 'Baba Ubaya' kuonyeshwa kadi nyekundu ikiwa ni njano mbili katika dakika ya 79.
Mabao mengine ya Mtibwa yalifungwa na Salum Kihimbwa dakika ya 24, wakati  la pili lilipachikwa na Issa Rashid 'Baba Ubaya' dakika ya 37.
Singida United ilipata mabao yake kupitia Salum Chuku na Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu na kufanya matokeo kuwa 2-2 kabla ya Mhesa kumalizia hilo la tatu la ushindi.
WAONDOKA SH 50
Mabingwa hao wapya wa Kombe la FA wamejinyakulia kitita cha Sh50 milioni na mshindi wa pili Singida United ilipata Sh 10 milioni.
MaoniMaoni Yako