Monday, June 11, 2018

Mkutano wa nchi za maziwa makuu kuhusu makosa ya jinai waanza Dar es Salaam

 

Balozi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya nchi za Maziwa Makuu Said Djinnit (kushoto)
Mkutano wa ngazi ya juu wa Jumuia ya nchi za Maziwa Makuu unaohusu ushirikiano katika masuala ya makosa ya jinai, umeanza hii leo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo wawakilishi kutoka nchi mbali mbali wanahudhuria.
Lengo kuu la mkutano huo ni pamoja na kubadilishana taarifa za kesi mbalimbali na kubadilishana watuhumiwa wanaokamatwa katika nchi nyingine.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili, Balozi Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya nchi za Maziwa Makuu Said Djinnit amesema kuwa viongozi wa eneo la Maziwa Makuu wameazimia kupambana na suala la wahalifu kuepuka adhabu, hivyo kuimarisha ushirikiano wa kimahakama kama njia moja wapo ya kupunguza uhalifu katika eneo hilo.
"Mbali na jitihada zinazofanyika kitaifa, bado kuna wahalifu ambao hawajakamatwa. ''Kwa masikitiko hakuna ushirikiano wa kutosha wa kimahakama baina ya nchi wanachama, matokeo yake, hawa watuhumiwa bado wako huru," amesema balozi Djinnit.
Wajumbe wa mkutano wa jumuia ya nchi za maziwa makuu
Wajumbe wa mkutano wa jumuia ya nchi za maziwa makuu
Kwa upande wake, Fredrick Manyanda ambae ni mkurugenzi msaidizi wa mashtaka amesema kikubwa kitakachojadiliwa ni namna ya kuimarisha ushirikiano.
"Makosa mengi yanayofanyika siku hizi yanafanyika kwa kuvuka mipaka, kwa hiyo ni lazima nchi zishirikiane, kuweza kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka ya nchi. Kuwepo urahisi wa kuvuka mipaka ndio kunasababisha urahisi wa wahalifu kuvuka mipaka kutoka nchi moja kwenda nyingine, kwa hiyo lazima kuwe na ushirikiano," amesema Manyanda.
Mkutano huo unatarajiwa kutoka maazimio ya namna ya kutekeleza mikataba na makubaliano yaliyopo ya ushirikiano katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Mkutano huu ni wa pili kufanyika, wa kwanza ulifanyika mwezi Novemba mwaka jana mjini Khartoum, nchini Sudan.

No comments:
Write comments

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();

Facebook