Mahakama kuchekecha Simba

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi wa kuifuta au la, hati ya mashtaka yenye washtakiwa ambao hawajakamatwa akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia HansPoppe na mwenzake dhidi ya tuhuma za kughushi nyaraka za kutakatisha fedha.

Mbali na HansPoppe,mshtakiwa mwingine ambaye hajakamatwa ni Franklin Lauwo. Wote wameunganishwa na vigogo wawili wa klabu hiyo, Evans Aveva na Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya aliyepangiwa kusikiliza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa na udhuru wa kikazi.
Washtakiwa hao waliunganishwa katika kesi hiyo ya kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.
Mei 14 wakili wa utetezi Nehemiah Nkoko aliwasilisha hoja ya kwamba haikuwa sahihi kwa mahakama kupokea hati ya mashitaka wakati washitakiwa wawili hawapo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mwandamizi, Leonard Swai ulipinga hoja za utetezi kwamba mahakama ilishaikubali hati ya mashitaka na washtakiwa waliopo waliweza kusomewa na kuamriwa kesi itasikilizwa baada ya washitakiwa wengine kupatikana.
Hata hivyo Hakimu Simba alipanga kutoa uamuzi Mei 28, mwaka huu lakini tarehe hiyo hakimu alisema bado hajamaliza kuandika uamuzi.
Katika kesi ya msingi, vigogo hao wanakabiliwa na mashitaka 10 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji fedha haramu.  
Aveva na Kaburu wapo mahabusu tangu Juni 29, mwaka jana kesi hiyo iliposomwa kwa mara ya kwanza kwa kuwa makosa ya utakatishaji fedha hayana dhamana kisheria.
MaoniMaoni Yako