Luis Enrique akaribia kutua chelsea


Kocha wa zamani wa timu ya Barcelona, Luis Enrique, anatajwa kuwa kocha mpya wa timu ya Chelsea, kurithi nafasi ya Antonio Conte, ambaye inasemakana ataondoka klabuni hapo kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu England 2018/2019.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, limeripoti kuwa vyombo vya habari nchini Hispania leo Juni 3, 2018 vimedai kuwa Enrique ambaye hana timu kwasasa atatambulishwa kujiunga na klabu ya Chelsea siku chache zijazo katika uwanja wa Stanford Bridge.
Taarifa za gazeti hilo zimeongeza kuwa klabu ya Chelsea imevutiwa na Luis Enrique kwasababu ni kijana na pia wanaamini kocha huyo ataiwezesha klabu hiyo kufuzu mashindano ya klabu Bingwa Ulaya kutokana na mbinu zake bora za ufundishaji.
Awali kulikuwa na taarifa za klabu ya Chelsea kuhusishwa na makocha Laurent Blanc kocha wa zamani wa PSG na kocha aliyemaliza muda wake katika klabu ya Napoli, Maurizio Sarri lakini Enrique anapewa kipaumbele zaidi kuteuliwa kuwa kocha wa klabu hiyo iliyopo jijini London
Luis Enrique amewahi kuifundisha klabu ya FC Barcelona kutoka Hispania katika kipindi cha miaka mitatu na kuiwezesha klabu hiyo kushinda jumla ya mataji tisa, likiwemo kombe moja la mashindano ya klabu bingwa Ulaya mwaka 2015.