Monday, June 4, 2018

Lugola aibua sakata hekalu la Rwakatare

 

NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, amesema serikali inaendelea na uchunguzi ili kubaini watu ambao nyumba zao zimejengwa kwenye fukwe kama ilivyo kwa Mbunge wa Viti Maalum,  Mchungaji Getrude Rwakatare, ili kuchukua uamuzi wa pamoja.
Nyumba ya Mchungaji Rwakatare ilitakiwa kubomolewa katika oparesheni ya ubomoaji wa majengo yaliyo ndani ya mita 60 kutoka mabonde ya Mto Msimbazi na Mto Mbezi na mengine yaliyo katika viwanja vya wazi.
Hata hivyo,  Mchungaji  Rwakatare  aliweka zuio mahakamani akipinga nyumba yake kubomolewa.
Lugola alisema tayari Baraza la Taifa la Hifadhi na Uzimamizi wa Mazingira (Nemc) limeanza kushughulikia jambo hilo kwa kushirikiana na Halmashauri ili kujua ukubwa wa tatizo hilo na serikali itachukua hatua baada ya kukamilisha suala hilo.
“Tumeanza katika mikoa ya Tanga na Mtwara ili tuwajue wenye tatizo kama la Mama Rwakatare, wako wangapi kwenye fukwe na maziwa yote tuliyo nayo kwa kuzingatia mita 60 ili tujue ukubwa wa tatizo,” alisema.
“Nimekuja na mtazamo tofauti, isije kuonekana kama anawindwa mtu mmoja wakati wenye makosa wapo chungu mzima. Sasa ili asionekane mtu mmoja anawindwa, tumeamua kuchukua kesi ya Mama Rwakatare kuzunguka na kubaini na wengine,” alisema.
Aidha, alisema kazi hiyo inaendelea nchi nzima na watapata taarifa ya kina kuhusu ukubwa wa tatizo hilo.
“Tukimaliza uchunguzi wetu serikali itachukua hatua kulingana na hali halisi kwa kuzingatia sheria ya mita 60 badala ya kumwangalia Mama Rwakatare peke yake ndiyo maana nimesema sitaki kushughulika na mtu mmoja. Nataka  niwabaini wale wote wenye tatizo kama hili,” alisema.

No comments:
Write comments

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();

Facebook