Monday, June 4, 2018

Babu wa miaka 97 aomba huruma ya Rais Magufuli

 

MZEE Abdallah Msham Kitwanga (97) amemwomba Rais John Magufuli, kumsaidia kupata haki yake ya shamba ambalo Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi ilishampa haki baada ya kushinda kesi.
Kitwanga alishinda kesi hiyo namba 316 aliyoifungua dhidi ya mtu aliyekuwa amevamia shamba lake.
Akizungumza na Nipashe juzi, mzee huyo alisema baada ya shamba lake kuvamiwa, alifungua kesi mwaka 2010 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi dhidi ya mvamizi huyo na mwaka 2015 mahakama ilitoa hukumu kwa yeye kushinda.
Pamoja na kushinda kesi hiyo hadi sasa, ameshindwa kuliendeleza kutokana na vikwazo anavyokumbana navyo. 
Kitwanga alisema mbali na kupata vikwazo kutoka kwa mtu aliyevamia shamba lake, pia anakumbana na vikwazo kutoka Manispaa ya Kinondoni ambako hawataki kumpa kibali cha ujenzi kwa kumpa masharti ambayo yako nje ya uwezo wake.
Alisema licha ya Mahakama Kuu kumwandikia barua yenye kumbukumbu namba LD/S.10/9/82 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni ikimtaka kumsaidia mzee huyo kulitumia eneo lake kwa kutobughudhiwa, mpaka sasa bado anasumbuliwa. 
Kitwanga alisema anaishukuru mahakama kwa kumpa haki yangu lakini anashindwa kuitumia kutokana na fujo anazofanyiwa na mvamizi aliyemshinda mahakamani na pia manispaa inashirikiana na mvamizi huyo kwa kumpa mashrti magumu ya kupata kibali cha ujenzi. 
"Kwa kweli nimehangaika sana pamoja na uzee wangu, hivyo namwomba Rais wangu Magufuli, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wanisaidie nipate haki yangu maana nateseka sana wakati haki ni yangu nilishapewa na mahakama, " alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Madale ambako ndipo shamba hilo lilipo, Gration Mbelwa, alisema anaushangaa uongozi wa manispaa kwa kukataa kumpa kibali cha ujenzi mzee huyo wakati shamba ni mali yake.
"Serikali ya mtaa inamtambua Mzee Kitwanga kuwa ndiye mwenye shamba hilo na mvamizi aliyekuwa amelivamia hatumtambui ndiyo maana tunashangaa kwa nini hapewi kibali cha ujenzi. Inakuwaje manispaa kusita wakati mahakama ilishathibitisha hilo?, " alihoji Mbelwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Kugurumjuli Titus, alisema manispaa inaheshimu uamuzi ya mahakama hivyo haiwezi kumnyima kibali cha ujenzi mzee Kitwanga kama anavyolalamika.
Mkurugenzi alisema Mzee Kitwanga aandike barua ya kuomba kibali cha ujenzi aambatanishe na hukumu ya kesi iliyompa ushindi kisha aipeleke kwa ajili ya taratibu za kupatiwa kibali.

No comments:
Write comments

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();

Facebook