Zijue balaa za radi, namna iIivyo hatari kwa wanaume

RADI inatokana na kuachiliwa kwa umeme tuli, tukio linalotokea kutokana na tofauti ya nguvu za umeme kati ya mawingu na ardhi.
Huwa ni cheche kubwa ya umeme kutoka angani yenye nguvu kubwa. Inaweza kusababisha moyo wa binadamu kuzima na hata kuacha kupiga, pia kuunguza viungo muhimu mwilini.
Wakati mvua zinaponyesha, huwa ni kawaida kwa radi kutokea, kila mwaka watu hufa katika maeneo mbalimbali duniani, baada ya kupigwa na radi.
Mwezi Machi mwaka huu, nchini Rwanda jumla ya watu 16 waliuawa radi iliyopiga kanisa moja la Kidventista Kusini mwa nchi hiyo na waumini 140 walijeruhiwa.
Pia, jumla ya wanafunzi 18 walijeruhiwa baada ya kupigwa na radi na mmoja wao alifariki.
Inakotokea
Mara nyingi radi hutokea kwenye sehemu ya chini ya anga, ambayo kwa Kiingereza hufahamika kama 'troposphere'.
Huwa inaenea kutoka kwenye wingu moja hadi jingine, hadi kufukua ardhini.
Radi inaweza pia kupatikana katika mawingu ya majivu kutokana na volkano.
Wanaume hatarini
Taasisi ya Serikali ya Kuzuia Ajali Uingereza (Rospa), inaeleza kuwa wanaume wana uwezekano mara nne zaidi ya wanawake kupigwa na radi.
Hiyo inadhaniwa inatokana na aina ya shughuli ambazo wanaume hujihusisha nazo, hivyo uwezekano wao kuwa nje wakati wa mvua ni mkubwa zaidi.
Wanaofanya michezo ya nje kama vile gofu mara nyingi wanaelezwa kuwa hatarini zaidi, kwani ndio wanapatikana katika maeneo ya wazi mbali na nyumba au sehemu za kujikinga mvua.
Aina tatu za ‘mikito’
Kutajwa kuna aina kuu tatu za radi ambazo zinaweza kumpiga mtu.
Moja, ni kupigwa moja kwa moja. Hapo radi inapiga kwa nguvu za umeme zinazopitia mwilini hadi ardhini.
Pili, ni kupigwa pembeni. Huwa ni kitu kilicho karibu na mtu anayepigwa na radi, nguvu inayoruka na kumfikia.
Tatu ni radi inapopiga ardhini na kisha kumfikia mntu.
Utajikingaje?
Tafuta hifadhi mahali kuna jumba kubwa au ndani ya gari. Kukiwapo jumba linalofaa mtu kujikinga dhidi ya radi, mtu unakuwa salama zaidi.
Usiwe katika maeneo ya wazi, au kwenye mlima ulio wazi.
Iwapo utakosa mahali pa kujikinga mvua, punguza uwezekano wako wa kupigwa kwa kujikunyata na kujifanya mdogo zaidi.Unaweza kuchutama, kuweka mikono yako kwenye magoti na kufichwa kichwa chako ndani.
Usijikinge mvua chini ya miti.
Iwapo upo mahali ambapo kuna maji, ondoka na kukwepa maeneo ya ufukweni yaliyo wazi.
Utafiti umeonyesha kwamba kuwa karibu na maji, kunaongeza hatari ya mtu kupigwa na radi.
Kwa kuwa radi huua nguvu za umeme, unafaa kujiepusha na vitu vya chuma vyenye ncha kali ukiwa kwenye mvua.
Inaelezwa, hatari ya mtu kupigwa na radi inaweza kuwapo kwa muda hata baada ya mvua kubwa kuacha kunyesha. 
MaoniMaoni Yako