Yondani aigomea Kamati TFF


BEKI wa Yanga, Kelvin Yondani ‘Vidic’ amegomea wito wa Kamati ya Nidhamu iliyomwita kabla ya kutoa maamuzi ya tukio la utovu wa nidhamu alilofanya kwenye mchezo wa watani wa jadi, Aprili 29.
Yondani anayeichezea Yanga kwa mwaka wa sita sasa, anakabiliwa na kosa la kinidhamu la kumtemea mate beki wa Simba, Asante Kwasi kwenye mchezo ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, alisema Yondan alishindwa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Nidhamu bila taarifa yoyote na sasa wamempelekea barua nyingine ya wito kabla ya kutoa hukumu dhidi yake. “Kamati inawajibika kutuma tena barua kwa mchezaji huyo wa Yanga kwa mara ya mwisho na kama asipotokea ina maana kamati itasikiliza upande mwingine na kutoa maamuzi,” alisema Ndimbo.
Kutokana na kosa hilo Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) ilimsimamisha Yondani na suala lake likipelekwa Kamati ya Nidhamu ambayo ipo kwenye mchakato wa kumchukulia hatua beki huyo.
Wakati huo huo, Kamati ya nidhamu imetoa hukumu kwa mchezaji wa Mbeya City, Ramadhani Malima ambaye aliingia uwanjani na kushangilia na wenzake kwenye mechi dhidi ya Yanga ya Aprili 22 wakati huo akiwa ameonyeshwa kadi nyekundu.
Credt: Mwanaspoti
MaoniMaoni Yako