Yanga yajipanga kuimaliza Rayon


KUFUATIA vipigo vya mfululizo walivyokutana navyo hivi karibuni, uongozi wa Yanga unatarajia kufanya kikao na  wachezaji wake kabla ya kuikaribisha Rayon Sports kutoka Rwanda katika ya hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa kesho itawakaribisha Rayon Sport katika mechi ya pili ya Kundi D itakayofanyika kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Hussein Nyika, aliiambia Nipashe kuwa hawataki kuona wanapoteza tena mchezo wa kesho ambayo unafanyika nyumbani, ndio maana wanajiandaa kupanga mikakati ya ushindi.
"Kikubwa tunataka kurudisha morali ya wachezaji wetu, tumevuliwa ubingwa wa Ligi Kuu, sasa tunaelekeza nguvu kwenye michuano ya kimataifa, tumepoteza mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya USM Alger, hatutaki kupoteza tena mchezo hasa kwenye uwanja wa nyumbani," alisema Nyika.
Yanga itaikaribisha Rayon Sports ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger  huku ikiwa inaburuza mkia kwenye msimamo wa Kundi D.

"MTIBWA WAMETUCHANGANYA"
Ikiwa tayari imeshavuliwa ubingwa, juzi Yanga ilikutana na kipigo cha tatu mfululizo kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo inaelekea ukingoni baada ya kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Kipigo hicho ambacho ni cha nne msimu huu kimeonekana kumchanganya kocha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Nsajigwa, alisema hakutegemea kupoteza tena mechi kwenye ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika ifikapo Mei 28 mwaka huu.
"Sijayafurahia matokeo haya, ila yameshatokea...matokeo yametuumiza,"alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 48 ikizidiwa kwa pointi nne na Azam inayoshika nafasi ya pili.
credit: Ipp Media
MaoniMaoni Yako