Yanga uwanjani kumalizia kiporo

LICHA ya kupoteza ubingwa wa msimu huu, Yanga inatarajia kucheza mechi ya 'kiporo' chake cha mwisho cha Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi kamili.
Mechi hiyo kati ya Yanga na Ruvu Shooting ni ya kulinda heshima kwa sababu timu zote mbili haziko kwenye janga la kushuka daraja huku Simba wakiwa tayari wameshatangazwa na kukabidhiwa kombe la ubingwa wa ligi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema jana kuwa kikosi chao kiko tayari kwa mchezo huo, na licha ya kufahamu wameshavuliwa ubingwa, watapambana kusaka ushindi ili kulinda heshima ya klabu yao.
Saleh alisema kuwa wachezaji wote wa timu hiyo wanafahamu umuhimu wa kuondoka na pointi tatu huku akimtaja mshambuliaji Donald Ngoma bado ni majeruhi na hataweza kucheza mechi hiyo.
"Maandalizi yanakwenda vizuri na katika mechi ya kesho (leo) tunatarajia kushusha kikosi kizima," alisema kwa kifupi Saleh.
Meneja huyo aliongeza kuwa wanafahamu changamoto walizokutana nazo ndani na nje ya uwanja katika msimu huu ni za kawaida katika mchezo wa mpira wa miguu na wanawaomba radhi mashabiki wao kwa kushindwa kuwapa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu.
Naye Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema kuwa hawaihofii Yanga na hiyo inatokana na kutokuwa na kiwango kizuri katika siku za hivi karibuni.
"Kwa namna ambavyo nimeitazama juzi (Jumanne), nina hakika tunauwezo mkubwa wa kuifunga Yanga, hawatutishi, wanafungika," alitamba Bwire.
Ligi hiyo ya Bara itamalizika Jumanne na tayari Njombe Mji imeshashuka huku ikisubiri kuungana na timu nyingine moja kuelekea Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Credit: IPP Media
MaoniMaoni Yako