Yanga umaskini ni wa kujitakia tu


WAKATI Klabu ya yanga ikipitia kipindi kigumu cha kuwa na hali mbaya ya kifedha, unaweza kusema kuwa katika hali hiyo kwa sasa ni kujitakia.

Matokeo inayopitia sasa Yanga ni ya kumtegemea mtu mmoja na hii baada ya mwenyekiti wake Yusuf Manji kujiondoa. Manji ndiye aliyekuwa akifanya kila kitu Yanga na hawakuwa wamejiandaa baada ya hapo.

Yanga sasa inahaha na kupita kipindi cha kukosa fedha hata za kulipa mishahara wachezaji wake kwa wakati. Mfumo wa Manji aliouacha ilikuwa ni kulipa mishahara mikubwa wachezaji wa klabu hiyo kiasi kwamba sasa inawapa wakati mgumu uongozi uliopo katika kulipa mishahara hiyo.

Pamoja na udhamini wa Kampuni ya SportPesa lakini bado Yanga inahaha kusaka fedha maana mahitaji makubwa kuliko inachopata.
Lakini huku ni kujitakia wenyewe Yanga maana kwa ukongwe wa klabu hiyo na wanachama ilionao leo siyo ya kulia njaa. Ni aibu kwa timu kubwa kama hiyo.

Yanga ilikuwa inatakiwa kujiendesha yenyewe na siyo kutegemea mtu. Leo ni aibu Yanga haiuzi jezi zake na ikanufaika, haiuzi hata vitu vyenye nembo yake. Wajanja wachache wamekuwa wakiuza jezi za klabu hiyo na kujipatia mapato huku klabu ikihaha kusaka mishahara ya wachezaji.

Leo hii Yanga inachekwa na watani wao Simba ambao mambo yanaonekana kuwaendea vizuri huku wakiwa katika hatua za mwisho kabisa klabu yao kuendeshwa kwa mfumo wa kisasa wa hisa.
Unaweza kujiuliza wale waliokuwa wakipiga kelele wakati ule wakati Yanga ikitaka kwenda hata katika mfumo wa kukodishwa wako wapi waokoe jahazi? Lakini jibu hakuna hata mmoja kwa sasa ambaye anajitokeza kusaidia kuokoa jahazi kwenye timu hiyo.
Yanga sasa wajipange kujitegemea baada ya kufanya makosa kwa kutegemea mtu muda mrefu sasa wajipange jinsi ya kujitegemea. Yanga inaweza kabisa kujiendesha. Ni kubadili mfumo na klabu iende kisasa tu ndiyo ukombozi wao.

Hakuna njia nyingine ya Yanga kujikwamua ni kusimama yenyewe kwa kupitia wanachama wake na kubadili mfumo. Mpira wa sasa ni pesa siyo kama zamani watu wanajitoa tu kwa mapenzi yao na kucheza. Angalia wachezaji wanagoma wengine wanaacha kwenda na timu hadi safari. Hii itoshe kuwapa somo Yanga kuwa mpira wa leo ni fedha.

Hakuna soka tena la kupeana moyo au kuelezana kuwa tuwe wazalendo, Yanga wanatakiwa kupitia kwenye haya wanayokutana nayo sasa kama funzo kwenye maisha yao.

Ni ngumu kuendesha soka kwa mfumo huu, ni lazima kila kitu kifanyike kwa mpangilio mzuri lakini wa mahesabu kwa kuwa kama Yanga hawataingiza fedha watapata wapi fedha za kulipa mishahara, posho za wachezaji na klabu hiyo wataiendesha vipi?

Nafikiri umefika muda wao sasa wa kutumia kipindi hiki kama funzo kwao.
Credit: Global Publishers
MaoniMaoni Yako