Wednesday, May 30, 2018

Waziri serikalini kumbadili jina msanii wa Bongo Fleva

TagsDar es Salaam: Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema atamtafutia jina lingine msanii wa bongo fleva,Claudia Lubao 'Chemical' kwa madai kuwa alilonalo halimpendezi.


Mwijage amesema hayo leo Jumatano, alipotambulishwa kwa msanii huyo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kitivo Cha Urithi wa Utamaduni, Dk. Eldidius Ichumbaki, katika maonyesho ya wiki ya utafiti, yanayoendelea chuoni hapo.


Ichumbaki amemweleza Waziri huyo namna wanavyomtumia Chemical na sanaa yake ya muziki katika kutangaza urithi mbalimbali unaopatikana nchini na kuonyesha video ya wimbo wa 'Kilwa Yetu'.


Baada ya kumaliza kuangalia wimbo huo, alimuuliza Chemical kwa mara nyingine kuwa kama ni yeye ameimba na kumweleza kuwa jina lake haliendani na alichoimba na kumwomba kama anaweza kumruhusu amtafutie jina lingine la kisanii.


"Yaani hukuona majina mengine hadi ujiite Chemical, Mimi hilo kwangu halijakaa vizuri na hii kazi unayoifanya hapa kwa kushirikiana na chuo kikuu, nitakutafutia jina lingine, si utaniruhusu?" Mwijage alimuuliza msanii huyo.


Kwa upande wa Chemical amesema, yupo tayari kupokea jina atakalopewa na Waziri japokuwa amekiri, jina la Chemical lililomtambulisha kwenye muziki kuliacha kabisa kwake itakuwa ngumu.


"Yaani hilo la Waziri lije tu nitalipokea, lakini huenda nikalitumia kama jina la pili kwani Chemical ndio jina nililolisotea kwenye muziki hadi leo najulikana," amesema Chemical.