Wasichana Wadogo Uingereza wanafanyiwa upasuaji wa Uke wao..

Wasichana wa umri mdogo nchini Uingereza wanafanyiwa upasuaji kurekebisha sehemu zao za uzazi kwa sababu hawapendezwi na muonekano wake, kipindi cha runinga cha Victoria Derbyshire kimefahamishwa.
Baadhi ya wasichana wanaanza kuitisha upasuaji huo wakiwa na miaka tisa pekee.
Dkt Naomi Crouch, ambaye ni mmoja wa wataalamu bingwa wa masuala ya uzazi, amesema ana wasiwasi kwamba wengi wa madaktari wa magonjwa ya kawaida wanaripoti visa vya wasichana ambao hawajabalehe wanaotaka kufanyiwa upasuaji kwenye uke wao.
Upasuaji huo ambao kwa Kiingereza hufahamika kama Labiaplasty, huhusisha kupunguzwa au kubadilishwa umbo kwa midomo ya uke wao.
Huduma ya Taifa ya Hospitali England (NHS) hupendekeza kwamba wasichana wasifanyiwe upasuaji huo hadi watimize miaka 18.
Lakini mwaka 2015-16, NHS wanasema wasichana zaidi ya 200 wa umri wa chini ya miaka 18 walifanyiwa upasuaji huo.
Wasichana zaidi ya 150 kati yao walikuwa wa chini ya miaka 15.
Dkt Crouch, ambaye ni mwenyekiti wa shirika la masuala ya uzazi na vijana wanaobalehe Uingereza anasema katika kipindi ambacho amefanyia kazi NHS, hakuwahi kukumbana na msichana ambaye alihisi kwamba anahitaji upasuaji huo.
"Wasichana wakati mwingine wataanza kusema, 'Naichukia, naomba iondolewe', na kwa msichana kuhusu hivyo kuhusu sehemu yake ya mwili - hasa sehemu nyeti hivyo kama ya uzazi - ni jambo la kusikitisha."
Kisa cha Anna
Anna - si jina lake halisi - alitaka kufanyiwa upasuaji wa labiaplasty akiwa na miaka 14.
"Nilipata wazo kutoka kwingine kwamba uke wangu haukuwa umekaa vyema vya kutosha au haukuwa wakupendeza na nilitaka upunguzwe.
"Watu wengi wa karibu ambao nilijumuika nao walikuwa wanatazama video za ngono na nilipata wazo kwamba uke unafaa kuwa umelainika na hakufai kuwa na kitu kinachojitokeza nje.
"Nilifikilia kwamba hivyo ndivyo kila mtu alivyokuwa, kwa sababu sikuwa nimeona picha za watu wa kawaida kabla ya hapo.
"Nakumbuka nikifikiria, 'Iwapo kuna upasuaji wa kurekebisha hili, basi ni wazi kwamba si mimi pekee ninaotaka kufanyiwa upasuaji, na labda halitakuwa jambo kubwa sana.'"
Baadaye alibadili msimamo wake na kuamua kutofanyiwa upasuaji.
"Sasa hivi, nafurahi sana kwamba sikufanyiwa upasuaji. Siuhitaji. Uke wangu ni wa kawaida. Asilimia mia kwa mia kawaida."

Paquita de Zulueta, daktari wa kawaida aliyefanya kazi kwa zaidi ya miaka 30, anasema ni miaka ya karibuni tu ambapo wasichana wameanza kwenda kwake wakianza kulalamika kuhusu muonekano wa uke wao.
"Nawaona wasichana wa miaka 11, 12, 13 ambao wanafikiria uke wao una tatizo - kwamba labda una umbo lisilo sahihi, ni mnene au mdogo sana, na wanakerwa sana nao.
"Wengi wanaamini kwamba midomo ya ndani ya uke wao haifai kuonekana, wanadhani uke unafaa kuwa kama mwanasesere au Barbie hivi, lakini uhalisia ni kwamba kuna tofauti kubwa sana katika muonekano wa uke wa wanawake. Ni kawaida kwa midomo ya ndani kujitokeza nje."
Analaumu picha ambazo si za uhalisia ambazo wasichana wengi wanakutana nazo kupitia video na picha chafu za ngono na pia kwenye mitandao ya kijamii.
"Hakuna elimu na uhamasisho wa kutosha na elimu hii inafaa kuanza mapema sana wakiwa wadogo, kuwaeleza wasichana kwamba kuna tofauti kubwa sana katika uke wa wanawake mbalimbali na - jinsi tulivyo tofauti kwa nyuso zetu - sote tuna tofauti huko kwenye sehemu nyeti, na hilo ni sawa."
NHS wanasema hawakufanya upasuaji huo kwa sababu za urembo bali ni kwa sababu za kimatibabu.
Kwa miaka kadha iliyopita, makundi ya madaktari wamekuwa wakiwatuma wagonjwa ambao wanahisi maumivu au wanakumbwa na mfadhaiko wakafanyiwe upasuaji.
Lakini Dkt De Zulueta anasema baadhi ya wasichana wanajua hilo na wamekuwa wakiongeza chumvi dalili zao kuhakikisha wanafanyiwa upasuaji.
"Wanafahamu kwamba wana uwezekano mkubwa wa kufanyiwa upasuaji iwapo watasema kwamba inawasumbua wakati wa kushiriki ngono na kushiriki michezo, wanajua hilo litaongezea uzito."
Dkt Crouch anaamini upasuaji huo unafaa kufanyiwa wasichana walio na kasoro ya kimaumbile inayoathiri afya yao.
"Inaniwia vigumu sana kuamini kwamba kuna wasichana 150 walio na kasoro ya kimaumbile inayoathiri afya yao kiasi kwamba walihitaji upasuaji kwenye uke wao," anasema.
Aliongeza kwamba upasuaji huo unakaribiana sana na ukeketaji, ambao ni haramu nchini Uingereza.
"Sheria inasema hatufai kufanya upasuaji huu kwenye miili ambayo bado inakua kwa sababu za kitamaduni. Utamaduni wa sasa wa nchi za Magharibi unaonekana kutukuza zaidi midomo midogo ya uke, ambayo pia haijajitokeza nje. Naona haya ni sawa (na ukeketaji)."
Visa vingi vya upasuaji kwa sababu ya urembo sana hufanywa na madaktari wa kibinafsi na kwa wasichana wa umri wa zaidi ya miaka 18.
Sekta hiyo imelaumiwa kwa kuifanya kuwa kama kawaida watu kufanyiwa upasuaji huo.
Mtaalamu wa upasuaji Miles Berry ametetea upasuaji huo na kusema unaweza kuimarisha maisha ya wanawake.
"Upasuaji huu unaweza kuwabadili watu kabisa, jinsi wanavyojihisi wenyewe, wawe wanajiamini zaidi na kuwa na motisha.
"Nimewaona wagonjwa wengi wa kati ya miaka 16 na 21 ambao hawajawahi kuwa na wapenzi kwa sababu wana wasiwasi kuhusu muonekano wa uke wao."
Chama kikuu cha wataalamu wa masuala ya uzazi Uingereza, kwa kimombo Royal College of Obstetricians and Gynaecologists, kinasema upasuaji huo haufai kufanywa hadi msichana awe amekomaa kabisa na viungo vyake kuacha kukua tena, baada yake kutimiza miaka 18.

Source: BBC swahili
MaoniMaoni Yako