Uhamiaji yaziamsha Simba, Yanga Bara

KUELEKEA msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2018/19, ambao utaanza Agosti mwaka huu, Idara ya Uhamiaji imezitaka Simba, Yanga na timu zote za hapa nchini kuhakikisha zinawaombea vibali wachezaji na makocha wake ambao wanatoka nje ya Tanzania.

Akizungumza na Radio One Stereo, Ofisa Habari wa Idara ya Uhamiani, Ally Mtanda, alisema klabu zote zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha mchakato wa kuwapatia vibali wageni wote kabla ya kuanza kucheza au kufundisha mpira.

Mtanda alisema agizo hilo linazihusu timu zote na si Simba na Yanga kwa sababu wanataka atakapowachukulia hatua wasiseme wameonewa.

"Tunapenda kuchukua nafasi hii kuzikumbusha timu zote za mpira wa miguu zenye waajiriwa kutoka nje ya Tanzania, kuomba vibali vya kufanyia kazi mapema, wasisubiri mpaka msimu mpya uanze, na hii si kwa ajili ya Simba na Yanga, ni kwa timu zote zenye wageni," alisema Mtanda.

Ofisa huyo aliongeza kuwa huu ni muda mwafaka kwa timu zote hasa zinazoshiriki Ligi Kuu Bara kukamilisha mchakato huo ili kuepuka usumbufu na kuwakosa wachezaji au walimu wao pale wanapowahitaji kuanza kutumikia ajira zao mpya.

Idara hiyo imetoa mwongozo huo ikiwa ni siku chake tangu kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu Bara 2017/18 ambao umeshuhudiwa Simba ikitwaa ubingwa wakati Majimaji FC na Njombe Mji zikishuka daraja.

Hivi karibuni Yanga ilishindwa kumtumia aliyekuwa kocha wake mkuu, George Lwandamina kutokana na kibali chake kumalizika na baadaye pia Mwinyi Zahera alikaa jukwaani kutokana na klabu yake hiyo mpya kutokamilisha taratibu za kupata kibali cha kufanya kazi nchini.

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, wao mbali na kupata vibali, pia hulazimika kulipiwa ada ya Sh. milioni mbili ambazo hupelekwa katika Mfuko wa Maendeleo wenye lengo la kusaidia kuendeleza wachezaji chipukizi.
MaoniMaoni Yako